NLD yaahidi kupitia upya mikataba ya madini

MONDULI, Arusha : MGOMBEA Urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, ameahidi kupitia upya mikataba yote ya madini ili kuhakikisha inakidhi matakwa ya wananchi. Alisema hatua yake ya kwanza itakuwa ni kubaini kwa uwazi faida zinazopatikana na taifa.
Doyo amesisitiza kuwa mikataba ya madini imekuwa ikifanyika kwa siri kwa muda mrefu, jambo ambalo atalivalia njuga ili rasilimali za Watanzania ziwe salama na zenye manufaa kwa wananchi.
Akiwa katika Kata za Makuyuni na Meserani, Wilaya ya Monduli, Doyo aliwaambia wananchi kuwa licha ya kuwa jirani na Wilaya ya Simanjiro yenye madini adimu kama Tanzanite, wananchi bado hawajanufaika ipasavyo. SOMA: NLD kuunganisha vijiji 5,000 maji ya bomba.
“Nimepita Makuyuni, nikawakuta ndugu zenu wakiuza pakiti za miwa na kina mama wakiuza bagia. Nikajiuliza, inaingiaje akilini kuona Watanzania wakiishi maeneo yenye migodi ya madini ya kipekee bado wakiendelea kuuza vipande vya miwa baada ya miaka 60 ya uhuru?” alisema Doyo.
Mgombea huyo amewaahidi wananchi kuwa endapo watamchagua, serikali yake itajenga viwanda vya kuongeza thamani ya madini ili wananchi wapate ajira zenye staha, badala ya kuendelea na biashara ndogo zisizo na tija huku wakiishi karibu na utajiri mkubwa wa Tanzanite.