Wagombea ubunge wajivunia miradi majimboni

TUNDURU : MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Fadhili Chilombe kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Wilaya ya Tunduru kuwa na umeme wa uhakika wa megawati 120.

Chilombe alitoa shukrani hizo wilayani Tunduru jana kwenye mkutano wa hadhara wakati wa kumuombea kura Mgombea urais kwa tiketi ya CCM,Samia Suluhu Hassan. Ameishukuru CCM kwa kumuamini na kumpa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama kugombea katika Jimbo la Tunduru Kusini.

Chilombe alisema kutokana na imani ya Rais Samia kwa wananchi wa Tunduru, kura zote za wananchi hao watamzawadia mgombea urais, wagombea ubunge  na wagombea udiwani wa CCM.Akitoa sera na ahadi  kwa wananchi, Chilombe alisema kitu kitakachosaidia wagombea wa CCM kupita kwa kishindo ni kutokana na fedha nyingi Rais Samia  alizomwaga katika wilaya hiyo kwa ajili ya kukamilisha mradi mkubwa wa umeme.

Alibainisha kuwa kutokana na matumizi madogo ya umeme unaofika megawati nne, mradi huo utasaidiaWilaya ya Tunduru kuwa na nyongeza ya umeme kwa sababu utazalisha megawati  120. “Mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 150 umeleta maajabu katika Wilaya ya Tunduru. Kama kuna watu wanataka kuona maajabu, waje Tunduru. Tunduru inaenda kuwa na umeme wa ziada wa megawati 116 kwa sababu sisi Tunduru tunatumia megawati nne,” alisema Chilombe.

Wakati huo huo mgombea ubunge katika Jimbo la Tunduru Kaskazini, Sikudhani Chikambo pia alimshukuru Rais Samia kwa kutatua changamoto kubwa ya mbolea iliyokuwa ikiwatesa wananchi kwa miaka mingi. Chikambo alitoa shukrani hizo jana wilayani Tunduru kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa CCM, Samia pamoja na wabunge na madiwani wa CCM.

Alisema ilifikia kipindi upatikanaji wa mbolea katika wilaya hiyo kuwa mgumu, kiasi cha wananchi kuiona bidhaa hiyo kuwa anasa na wengine kukata tamaa kuitumia. Aliongeza kuwa, kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na serikali chini ya Rais Samia, hivi sasa wananchi wananunua mbolea watakavyo muda wowote, akitolea mfano kuwa ununuzi wa mbolea sasa umekuwa kama soda.

Mwananchi anaamua na kuchagua aina ya soda atakayo wakati wowote. “Rais umefanya makubwa katika wilaya yetu kuanzia katika sekta ya elimu, afya, maji na Barabara. Mambo ni safi ikiwa ni pamoja na kilimo, ambapo wananchi wananunua mbolea kama soda, tofauti na zamani,” aliongeza. SOMA: Tanzania kuendeleza mapinduzi ya elimu

Kwa upande wa barabara, alisema serikali imedhamiria kuifungua Tunduru baada ya kuiweka barabara katika Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2025 hadi 2030, barabara ambayo ilikuwa kikwazo ya Mlingoto – Nalasi – Mchoteka hadi Mtwara Pachane yenye urefu wa kilometa 350.

Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, historia inaenda kuandikwa kwa kuchaguliwa mbunge mwanamke kwa mara ya kwanza katika majimbo mawili ya Wilaya ya Tunduru. Aliwaahidi wananchi wa Tunduru Kaskazini kuwa wakimchagua, atahakikisha kuwa ilani ya CCM inatekelezwa kikamilifu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button