Burkina Faso,Mali, Niger watangaza kujiondoa ICC

BAMAKO, Mali : NCHI za Burkina Faso, Mali na Niger, ambazo zinaongozwa na tawala za kijeshi, zimetangaza kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Mataifa hayo yamesema mahakama hiyo yenye makao yake The Hague, Uholanzi, ni chombo cha ukoloni mamboleo kinachotumiwa na mataifa makubwa kuwakandamiza.
Kwa mujibu wa viongozi wa kijeshi wa nchi hizo tatu, ICC imeshindwa kushughulikia ipasavyo kesi zinazohusu uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari barani Afrika, jambo lililopelekea kupoteza imani na mahakama hiyo. Wamesema sasa wanataka kuanzisha mifumo ya jadi ya kuhakikisha haki na amani.
Mahakama ya ICC ilianzishwa mwaka 2002 kwa lengo la kuwashtaki wahusika wa uhalifu mkubwa pale ambapo nchi husika zinashindwa au hazina nia ya kufanya hivyo. Hatua ya mataifa hayo ya Sahel inachukuliwa kama changamoto kubwa kwa taasisi hiyo ya kimataifa. SOMA: Mali, Burkina Faso wasusia kikao cha ulinzi