Zitto aahidi maendeleo pembezoni mwa mji wa Kigoma

KIGOMA: MGOMBEA ubunge wa Chama cha ACT Wazalendo Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema kuwa akiingia madarakani atatoa kipaumbele katika utekelezaji wa kupeleka maendeleo kwenye maeneo ya pembezoni ya miji ambako kwa sasa yameachwa nyuma kimaendeleo.

Kabwe amesema hayo akihutubia mkutano wa kampeni za ubunge katika jimbo hilo uliofanyika kwenye kata ya Businde manispaa ya Kigoma Ujiji na kusema kuwa hali ya kuachwa nyuma kimaendeleo kwa maeneo hayo kumeleta tofauti kubwa baina ya wananchi wa maeneo hayo na wale wa kati kati ya manispaa.

Mgombea huyo amesema kuwa moja ya sababu hiyo ni kutokuwepo kwa barabara za uhakika kuunganisha maeneo hayo na maeneo ya miji hivyo shughuli nyingi za kiuchumi zimedumaa na watu wengi hawataki kwenda kuwekeza huko kwa sababu ya changamoto hiyo ya miundombinu.

Amebainisha kuwa hata katika huduma za kijamii bado maeneo hayo yamekumbwa na changamoto ya uhaba mkubwa wa walimu ikiwemo Shule ya Sekondari Businde yenye walimu sita ambapo wazazi wanalazimika kuchanga Sh 6,000 ili kulipa walimu wa kujitolea.

Akizungumza katika mkutano huo, mgombea udiwani wa Kata ya Businde, Saidi Makala amesema kuwa watu wa eneo hilo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuporwa maeneo yao bila fidia kwa sababu diwani aliyekuwepo alikuwa akishirikiana na serikali katika uporaji huo hivyo kuomba wananchi wamchague ili awasimamie kuhakikisha maeneo yao hayaporwi kwa kigezo cha uwekezaji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button