Samia: Tutaendelea na kasi ileile

MCHINGA : CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Serikali ya Awamu ya Sita katika awamu yake ya pili itatekeleza miradi kwa kasi ileile ya awamu ya kwanza. Mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Samia Suluhu Hassan alisema hayo katika mkutano wa kampeni kwenye Jimbo la Mchinga mkoani Lindi.

Samia alisema serikali ya CCM itakamilisha miradi iliyoanza na ile ambayo imebainishwa kwenye ilani ya uchaguzi. “Hakuna chama kitakachoweza kwa sasa hivi kulinda na kuinua utu wa Mtanzania kama Chama Cha Mapinduzi na ndiyo maana tumekuja na hii Kaulimbiu ya ‘Kazi na Utu’.

Maana yake, tupeni ridhaa yenu Chama Cha Mapinduzi, tuendeshe nchi hii tena kwa miaka mitano ijayo,” alisema. Aliongeza: “Huko mbele tutakuja tena kufanya tathmini, tufanye kazi ili tuinue utu wa Mtanzania na katika kuinua utu wa Mtanzania ni kumpatia maji safi na salama, elimu, huduma za afya, umeme, kilimo.

Huo ndio kulinda na kuukuza utu wa mtu. Ukisoma ilani yetu yote tunakwenda kufanya kazi ya kukuza na kuulinda utu wa Mtanzania.” Samia alisema serikali itakeleza miradi ya maji, ukiwemo uchimbaji wa visima, kuhakikisha vijiji 10 vinapata huduma ya maji safi na salama. “Mwingine anakwambieni nitaleta maji, alikuwa wapi asilete siku zote.

CCM tumeshaleta maji. Kwa hiyo, ahadi zao ni za kuigiza tu. Niwaombe sana wananchi Oktoba 29 nendeni mkachague Chama Cha Mapinduzi,” alisema. Aliahidi kuendelea kutoa ruzuku za pembejeo, sambamba kutoa viuatilifu vya salfa na dawa bure kwa wakulima wa korosho.

“Tungemtaka mkulima afanye kila kitu, mazao yanayopatikana sasa yasingepatikana, mashamba yasingekuwa yanapewa huduma inavyotakiwa. Hivyo, tunatoa ruzuku ili wakulima wazalishe, wauze na kupata fedha. Huko mbele tutaangalia msimame kwa miguu yenu lakini kwa sasa tutaendelea kutoa ruzuku,” alisema.

Pia, Samia aliahidi kuendelea kutafuta masoko ya mazao na akasema mfumo wa stakabadhi za ghala umetoa matokeo mazuri katika kuimarisha bei ya mazao. “Mfumo wa stakabadhi ghalani ulikuwa mgumu kukubalika lakini umeleta matokeo mazuri kwa wakulima. Nataka niwahakikishie kwamba, kinacholetwa na serikali yenu mjue kina manufaa. Kikubalieni na mkifanyie kazI.

Pia, tunatoa huduma za kitaalamu, huduma za ugani kuwawezesha maofisa ugani waweze kufuatilia maendeleo ya kilimo chetu,” alisema. Samia alisema serikali imetoa Sh bilioni 30.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ya umwagiliaji maeneo ya Lutamba na Kilangala, ili wakulima walime mara mbili kwa mwaka.

Alisema serikali itaendelea kusimamia sekta ya kilimo, kwa sababu Tanzania inazalisha mazao kwa wingi, hivyo muhimu kuwepo upatikanaji masoko yenye uhakika. “Tunalisha majirani zetu, huko nyuma mbaazi hapa Lindi ilikuwa mboga lakini leo mbaazi ni zao la biashara na linaingia katika stakabadhi ghalani likileta bei nzuri. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya kilimo cha umwagiliaji, ili watu wazalishe mara mbili kwa mwaka. Kwa sababu hata mpunga ni zao la kibiashara.

Mpunga wetu upo nchi nyingi za Afrika Mashariki, hata Ulaya mchele wa Tanzania unapatikana,” alisema Samia. Alisema kwa kuwa wakulima huzalisha sana, litajengwa soko la kisasa la mazao likiwa na huduma za mazao ya mboga mboga ambayo pia yana soko nchi za nje.

Pia, Samia aliahidi kuendelea na ruzuku kwenye chanjo ya mifugo na kwenye ng’ombe na kuwa serikali imekuwa ikibeba nusu ya gharama. “Kwenye ruzuku ya chanjo, siyo Kitomanga na Mipingo peke yake, maeneo yote yenye ng’ombe tumesema tutatoa ruzuku ya chanjo. SOMA: Samia atoa uhakika mradi kuchakata gesi

Kama chanjo inalipiwa Shilingi 20,000, mfugaji atalipia Shilingi 10,000, kama ni Shilingi 30,000 mfugaji atatoa 15,000 na serikali itamalizia,” alisema. Aliongeza: “Lakini kwa upande wa kuku, chanjo zote ni bure. Twende tukachanje mifugo yetu, kwani madhumuni ya kuchanja ni kwamba kwa muda mrefu tulikuwa tukihangaika kutafuta soko…

Tumetoa ruzuku ya chanjo ili mifugo yote ya Tanzania itambulike na tuweze kuingia katika soko la kimataifa”. Pia, Samia alisema serikali itajenga majosho na machinjio ya mifugo, ili nyama ya Tanzania iwe na viwango vinavyotambulika maeneo mbalimbali duniani. Kwa upande wa uvuvi, alisema serikali ilitoa mikopo ya boti za kisasa za uvuvi zenye thamani ya Sh milioni 712, wakati awamu ijayo serikali itaendelea kutoa boti na vifaa vya uvuvi.

Pia, Samia alisema katika maeneo ya Mkoa wa Lindi, huduma zote za afya zinapatikana zikiwemo za kibingwa, baada ya uwepo wa hospitali kubwa ya rufaa. “Kwa bahati nzuri, jirani zenu wa Mtwara wanapata huduma za kibingwa, kwa hiyo kwa Ukanda wa Kusini masuala ya afya yapo vizuri sana.

Tutaendelea na kasi ileile,” alisema. Samia alisema akichaguliwa, serikali yake itaongeza kasi ya kujenga nyumba za walimu. “Mchinga ni eneo lililochaguliwa kuwa na shule maalumu ya mchepuo wa sayansi kwa wasichana. Changamoto ndogo walizokuwa nazo tumeziondoa, kwa hiyo matumaini yangu kwamba wataendelea kusoma vizuri,” alisema. Samia alisema serikali imeanzisha Shule ya Ufundi Stadi ya Jakaya Kikwete, iliyopo Kata ya Nangaro ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 70.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button