Iringa yazindua uhakiki wa Anwani za Makazi

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amezindua rasmi zoezi la uhakiki wa taarifa za anwani za makazi katika Manispaa ya Iringa, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa serikali kutoa huduma bora na za haraka kwa wananchi katika zama za uchumi wa kidijitali.

Sitta alisema uzinduzi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa mwaka 2022, ya kuimarisha utambuzi wa makazi na kuweka mazingira wezeshi ya kunufaika na fursa za uchumi wa kidijitali.

“Ili serikali iweze kutoa huduma za dharura kwa ufanisi kama magari ya wagonjwa, zimamoto au huduma za usalama, ni lazima tujue mahali halisi wananchi wanapoishi kupitia namba za nyumba, majina ya barabara na postikodi,” alisema Sitta.

Kwa mujibu wake, mkoa wa Iringa tayari umesajili anwani 327,991, sawa na asilimia 124 ya lengo la 273,920, katika mfumo wa kidijitali wa anwani za makazi (NaPA).

Aidha alisema, vibao 2,245 vya namba za nyumba vimebandikwa na nguzo 2,759 zenye majina ya barabara zimesimikwa.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Tamisemi, Mashaka Makuka, alisema mfumo wa NaPA ni mageuzi makubwa kwa utawala wa vijiji na mitaa kwani unawezesha utambuzi wa wakazi kwa haraka na kurahisisha utoaji wa huduma za utambulisho wa mkazi kidijitali.

“Kwa sasa barua za utambulisho wa mkazi zinaweza kutolewa moja kwa moja kupitia mfumo wa NaPA bila kutumia karatasi, jambo linalopunguza gharama na kuokoa muda wa wananchi,” alisema Makuka.

Makuka aliongeza kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi tayari imeteua waratibu wa anwani za makazi kwa ngazi za mikoa na wilaya ili kuhakikisha mfumo huo unaboreshwa na taarifa zinaendelea kuwa sahihi.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bakari Mwamgugu, alisema mfumo huo uliosajili anwani milioni 12.3 tangu mwaka 2022, tayari umeonesha manufaa kwa taifa.

Alitaja mifano ya jinsi taarifa za anwani zilivyosaidia kutambua waathirika wa maporomoko ya tope Hanang na mafuriko katika wilaya za Rufiji na Kibiti, hivyo kurahisisha shughuli za uokozi na urejeshaji wa hali.

Hadi kufikia Septemba 21 mwaka huu, jumla ya barua za utambulisho 668,558 zilitolewa kitaifa, huku katika Manispaa ya Iringa pekee barua 6,925 zikiwa zimeshakamilishwa.

Sitta aliwataka wenyeviti wa mitaa na watendaji wa kata kuhakikisha mafunzo ya siku moja kwa wenyeviti na siku mbili kwa watendaji yanafanyika kwa ufanisi, na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu.

“Tunataka kuona barabara zote za Manispaa ya Iringa zinakuwa na nguzo zenye majina ya mitaa. Mfumo huu ni daftari la kidijitali la wakazi na zoezi hili ni endelevu,” alisisitiza.

Alibainisha kuwa mfumo wa NaPA unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), na utakuwa chachu ya kupanga mipango ya maendeleo kwa usahihi.

Kwa wananchi wanaoomba mikopo ya elimu ya juu, Sitta alikumbusha kuwa sasa ni sharti kuwa na barua ya utambulisho wa mkazi kutoka NaPA, jambo linaloonesha namna mfumo huo unavyogeuka kuwa nyenzo ya msingi katika maisha ya kila siku.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button