Samia aahidi reli, barabara kupaisha uchumi Tanga

TANGA; MGOMBEA urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema serikali yake itajenga reli kuunganisha bandari ya Tanga na Musoma mkoani Mara.

Samia amesema reli hiyo itatoka katika bandari hiyo kuelekea Arusha hadi Musoma na itakuwa na urefu wa takribani kilometa 1,108.

Alisema hayo kwenye mkutano wa kampeni katika Viwanja vya Usagara, Tanga jana.

Samia alisema reli hiyo itafungua maeneo ya viwanda na madini na kuzidi kuongeza fursa za ajira katika Mkoa wa Tanga.

“Pamoja nayo ni Barabara ya Handeni hadi Singida, hii nayo tumeiunganisha na bandari sababu watakaojenga ni wenyewe Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa sababu ya urahisi wa kusafirisha mizigo yao. Kwa hiyo TANROADS (Wakala ya Barabara Tanzania) na bandari watasaidiana kujenga barabara hii,” alisema.

Samia alisema Bandari ya Tanga inaboreshwa na uamuzi waliofanya, ya kwamba Tanga ni bohari ya mafuta na gesi jambo ambalo litachangia kuzalisha ajira mpya nyingine 2,100 ndani ya mkoa huo.

“Hili linakwenda kunyanyua uchumi wa wana Tanga. Mbali na mradi huu, kama mnavyojua tuna miradi mingine ya kimkakati inayofungamana na bandari hii pia,” alisema.

Aliitaja miradi hiyo ni ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kati ya Uganda- Hoima nchini Uganda na Chongoleani mkoani Tanga (EACOP).

Samia alisema mradi umekamilika kwa asilimia 84 na kuleta manufaa mengi.

“Mfano tayari eneo la Chongoleani pekee watu 1,300 wameajiriwa na mradi huu na ndani ya Wilaya ya Tanga watu 200 wameajiriwa kwenye mradi huu,” alisema.

Samia alisema mwelekeo wa serikali ya CCM kwa ujumla ni kuirejesha Tanga ya viwanda kama sehemu ya mkakati wa kitaifa kwa kuijenga Tanzania ya viwanda kwa kuanzisha na kuendeleza kongani za viwanda katika kila wilaya.

“Sambamba na hilo, tutafufua viwanda vilivyobinafsishwa lakini havijaendelezwa, ikiwemo Kiwanda cha chai Korogwe lakini pia nimefurahi kuona Kiwanda cha Foma nacho kimefufuliwa pia kiwanda cha saruji kimeongezewa uwezo wa uzalishaji, sasa Tanga inaleta saruji nyingi kuliko ilivyokuwa kabla. Pia, kuna kiwanda cha kufunga magari ya wagonjwa kinakuja hapa Tanga,” alisema.

Samia alisema serikali yake itaendelea kuvuta wawekezaji ili wawekeze kwenye maeneo ya viwanda Tanga na kutoa wito kwa wana Tanga kuwa maeneo ambayo hayatumiki na yako mikononi mwa watu yarudishwe, ili wanaokuja kutaka maeneo ya viwanda wakute yako tayari.

Aidha, alisema watafanya upanuzi na ukarabati mkubwa katika Barabara ya Dar es Salaam-Chalinze-Segera-Arusha.

“Na hizi ni kilometa 646 tunakwenda kuzitanua sababu ya msongamano, iko ndani ya ilani na tunakwenda kuifanyia kazi… Ahadi yetu wana Tanga ni kuikamilisha miradi inayounganisha mikoa ya Tanga na Pwani na itakayochangia kubadilisha kabisa uchumi wa Ukanda huu wa Pwani,” alisema Samia.

Alisema ili kukuza ajira za vijana, serikali imekuja na Mpango wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kwenye maeneo ya kilimo, madini na uvuvi.

“Kwa hapa Tanga, tunakuja kwenye maeneo ya kilimo na madini. Kwenye sekta ya madini tumeanzisha masoko manne ya dhahabu na vito, hatua inayowavutia wawekezaji lakini pia wachimbaji wadogo waweze kuchimba kwa kiasi kikubwa na kwa kweli hapa Tanga tumetoa leseni kwenye maeneo ya Ilozo, Kimang’a, Kipungwi, Mikunguni, Mwera na Tungamaa. Upelekaji wao wa dhahabu kwenye masoko umeongezeka kwa kiasi kikubwa,” alisema Samia.

Aliongeza: “Tutaendelea kuweka nguvu hapo na kupima maeneo mengine ili vijana wetu waingie kwenye uchimbaji, wajiajiri, waajiriwe na maisha yaendelee”.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. JOIN US Everybody can earn 250/h Dollar + daily 1K… You can earn from 6000-12700 Dollar a month or even more if you work as a part time job…It’s easy, just follow instructions on this page, read it carefully from start to finish… It’s a flexible job but a good earning opportunity. tab for more detail thank you……..
    .
    This is my main concern……………………………………. http://Www.Cash43.Com

  2. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
    .
    M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us→→→→→→→→→→ http://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button