Mfumo wa stakabadhi ghalani utasimamiwa

MTWARA : CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kuendelea kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa wakulima. Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira alisema hayo alipozungumza na wana CCM mkoani Mtwara.

“Wapo watu wanapinga stakabadhi ghalani bila kujua, mimi najua. Miaka ile nikiwa Waziri wa Kilimo, mimi nilikuja hapa. Mkulima wa korosho alikuwa analipwa Shilingi 300, tena siyo kwa kipimo cha kisasa, analipwa Shilingi 300 kwa kitu kinaitwa ‘kangomba’, mnajua kangomba?” Alihoji.

“Ni kipimo ambacho ni zaidi ya kilo na wanalipwa 300, katikati yuko mtu mwingine anayenunua kwa kangomba, halafu anaenda kwa mwenye pesa yeye anamuuzia Shilingi 500. Hana mkorosho hata mmoja lakini yeye anapata Shilingi 200, mwenye mkorosho aliyenunua salfa analipwa 300. Tajiri wa kihindi anazipeleka moja kwa moja mpaka India yeye analipwa Shilingi 2,000 mpaka Shilingi 3,000 lakini mkulima wa korosho hizo hata viatu anashindwa kununua”.

Wasira alisema sasa bei ya korosho safi Mtwara inafika hadi Sh 4,000 kutoka Sh 300, ikiwa ni kazi ya CCM. Wasira alisema maendeleo ni msingi wa tatu wa CCM na kwamba kila miaka mitano kinaeleza ilani yake inakuaje.“Hapa Mtwara wakulima wa korosho ingawa hapa ni mjini lakini hawa ni walewale tu. Wakulima wa korosho wanapata salfa bila ya malipo au siyo? Kuna chama kinajua salfa hii zaidi ya CCM? Vingine vinababaisha tu,” alisema.

Wasira alisema katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025-2030k, endapo kitapewa ridhaa kitaisimamia serikali kujenga kongani ya viwanda kwa ajili ya kubangua korosho. “Tumejenga madarasa mapya 35 mjini peke yake, siyo Mtwara nzima. Shule moja mpya kabisa imejengwa Mtwara, sekondari tumejenga tatu katika muda wa miaka minne, tumejenga madarasa ya sekondari 77 Mtwara Mjini na nyinyi hamkuchangishwa,” alisema Wasira. SOMA: Mwinyi: Pigeni kura Oktoba 29

Alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025-2030 imeelekeza kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi. “Kwanza tunataka kujenga vituo vipya vya afya hapa mjini, kwa sababu ya ongezeko la watu. Tutajenga zahanati 12 hapa mjini, tutajenga shule mpya za msingi tano, tutajenga madarasa ya msingi 42, tutajenga sekondari mpya nne hapa mjini na tutarekebisha madarasa saba” alisema Wasira.

“Vilevile, tutajenga sehemu ya chuo kikuu hapa Mtwara, kuna ujenzi wa soko utafanyika hapa, tunajenga stendi hapa Mtwara na tutajenga kongani ya viwanda kwa ajili ya kubangua korosho, hapa… tunataka korosho zinazozalishwa hapa ziende moja kwa moja soko la dunia zikiwa zimebanguliwa,” alieleza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button