Taifa Stars ijipange na AFCON Morocco

TAIFA Stars haina budi kubadili muelekeo wake na sasa wanapaswa kuwaza jinsi gani ya kujiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazoanza Desemba mwaka huu Morocco.

Kiuhalisia safari ya timu hiyo walau kupata nafasi ya mshindi wa pili bora kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwakani zitakazoandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico, imefikia kikomo.

Taifa Stars haina tena nafasi ya kupata nafasi ya mshindi wa pili bora, hivyo kuwa miongoni mwa timu nne kutoka Afrika zitakazocheza mechi za mchujo kuwa katika kinyang’anyiro cha kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.

Kama Taifa Stars haiwezi tena kupata nafasi ya mshindi wa pili bora, ikiwa ni baada ya kufungwa nyumbani bao  1-0 na Niger, basi mtazamo wao unapaswa kuwaza zaidi fainali za Mataifa ya Afrika.

Taifa Stars mara zote ilizoshiriki fainali hizo, kuanzia zile zilizofanyika Lagos, Nigeria mwaka 1980, haijawahi kuvuka hatua ya makundi.

Hapa ndipo wasimamizi wa timu hii kwa maana ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sambamba na Kocha Mkuu wake, Hemed Suleiman ‘Morocco’ wanapaswa kufikiria zaidi namna gani itafanya vile kwenye fainali za Mataifa ya Afrika zitakazoandaliwa na Morocco mwishoni mwa mwaka huu.

Kitendo cha timu hiyo kufika robo fainali ya michuano ya Mabingwa wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) kama mmoja wa nchi waandaaji, kinapaswa kuwa deni kwao kuona namna gani watafanya vizuri zaidi kwenye Afcon, Morocco.

Kwa hiyo hata hizi mechi zilizosalia za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa Taifa Stars zinatakiwa zibebe taswira ya maandalizi yao kwa ajili ya Afcon.

Taifa Stars imebakiwa na mechi dhidi ya Zambia, Oktoba 8 mwaka huu Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, Zanzibar.

Hata kama watashinda mchezo huo hawatakuwa moja ya washindi wa pili bora, hivyo kutakiwa kucheza mechi za mchujo za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia.

Kama ndivyo, mbali na kuwa ni mchezo wa kulinda heshima zaidi, mtazamo wao unapaswa kwenda mbali,
kuuchukulia kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya Afcon itakayofanyika Morocco.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button