GNU ya Zanzibar, alama ya amani

KASKAZINI PEMBA : MGOMBEA wa urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema kuwa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ni matokeo ya busara na uvumilivu wa wananchi waliotanguliza amani na umoja wa taifa.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Jimbo la Gando, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Othman alisema kwa zaidi ya miaka 30 wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakiridhia matokeo ya uchaguzi kwa lengo la kulinda amani na kuendeleza maendeleo ya nchi.

Othman alisisitiza kuwa kudai mabadiliko kupitia sanduku la kura ni njia sahihi ya kidemokrasia, na kwamba kila chama kinapaswa kuwa tayari kukubali matokeo halali yatakayotokana na uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu. Aliongeza kuwa ni wakati wa CCM kujitayarisha kuwa mshiriki wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa endapo haitashinda, jambo ambalo ni halali kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Mgombea huyo alisema serikali yake itahakikisha rasilimali zote za nchi, ikiwemo ardhi, bahari, mafuta na kilimo, zinawanufaisha wananchi wa Zanzibar. Pia aliahidi kuimarisha ajira, kupambana na rushwa na kuweka mazingira bora ya maisha kwa kila familia. SOMA: Ilani NCCR-Mageuzi, ACT Wazalendo, AAFP na ajenda ya kukuza uchumi

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo na Meneja wa Kampeni wa mgombea huyo, Mansoor Yussuf Himid, alisema uongozi wa Othman Masoud utaipeleka Zanzibar katika zama mpya za amani, usawa na haki kwa wananchi wote bila kujali itikadi za kisiasa. Aliongeza kuwa hali ya hofu na mgawanyiko katika jamii inaweza kuisha iwapo wananchi watampigia kura nyingi Othman katika uchaguzi ujao.

Aidha, Mansoor aligusia changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZAN ID), akisema ni haki ya kila Mzanzibari kuwa navyo, na hivyo akaomba serikali kuhakikisha hakuna ubaguzi wa kisiasa katika utoaji wa vitambulisho hivyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button