Waislamu washauriwa kutoandamana Oktoba 29

DAR ES SALAAM: WAUMINI wa Dini ya Kiislamu wameshauriwa kutoshiriki maandamano yanayohamasishwa kwenye mitandao ya kijamii yaliyopangwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu, na badala yake wajitokeze kupiga kura kwa amani katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe hiyo.
Wito huo ulitolewa jana Oktoba 4,2025 na Shehe wa Msikiti wa Mtambani, Wilaya ya Kinondoni mkoa wa Dar es salaam,Shabani Pembe wakati wa Kongamano la Kuombea Uchaguzi, Amani na Dua ya Nchi lililofanyika jijini Dar es Salaam.
“Hakuna muislamu yeyote atakayeingia barabarani kuandamana. Atakayeingia barabarani Oktoba 29 atakutana na mambo yasiyoridhisha na kuipa familia yake shida. Wanaohamasisha maandamano hawapo nchini, hivyo ni heri mkapige kura badala ya kuandamana,” amesema Shehe Pembe.
Shehe huyo alisisitiza kuwa waislamu hawapaswi kushiriki maandamano yenye kuashiria uvunjifu wa amani, bali washiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia kwa njia ya amani.
Akitoa mada katika kongamano hilo, Shehe Othman Singa aliwataka Watanzania kuondoa dhana potofu kuwa uchaguzi ni kinyume na mafundisho ya Kiislamu.
“Uchaguzi ni jambo linalotambulika katika Uislamu. Kupiga kura ni haki yetu; usipokwenda kupiga kura maana yake unamwachia mwingine akuchagulie kiongozi. Hivyo nendeni mkapige kura, mchague kiongozi atakayewakilisha maslahi yenu,” amesema Shehe Singa.
Aliongeza kuwa uchaguzi unahitaji amani, akisisitiza kuwa kila muislamu anapaswa kuwa balozi wa amani, kwani amani ni tunu muhimu inayopaswa kulindwa kwa hali zote.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, aliwataka waumini kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.
“Amani ni tunu muhimu kwa Watanzania. Tuendelee kuilinda kwa nguvu zote na tujitokeze kwa wingi kupiga kura. Dk Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa na inayoonekana, hivyo anastahili kuendelea kuongoza,” amesema Chatanda.
Mgombea Ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kibamba, Angella Kairuki alipongeza Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Ubungo kwa kuandaa kongamano hilo lenye kauli mbiu ya “Amani katika Uchaguzi”, akisema limekuwa chachu ya mshikamano na utulivu.
“Uchaguzi utakuwa huru na wa haki. Viongozi wa dini mnahusika kuwahamasisha waumini kujitokeza kupiga kura, kwani usiposhiriki kuchagua, huna haki ya kulalamika. Amani na mshikamano ni nguzo muhimu za maendeleo,” amesema Kairuki.
Kairuki pia aliwaomba wananchi kumpa ridhaa ya kuongoza Jimbo la Kibamba, akiahidi kushughulikia changamoto za usalama, elimu kwa watu wenye mahitaji maalumu, na kuhakikisha shule maalumu zinapatikana katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando aliwahakikishia wananchi kuwa Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa amani, uwazi na uhuru, akiwataka wakazi wa Kibamba kujitokeza kupiga kura kwa utulivu.
“Uchaguzi ni fursa ya kidemokrasia. Chagueni viongozi watakaoleta maendeleo na kuwatumikia kwa uadilifu. Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wote watakaochaguliwa kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi,” amesema Msando.
Kongamano hilo, lililoandaliwa na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Ubungo, lililenga kuhimiza amani, mshikamano na ushiriki wa kidemokrasia kuelekea Uchaguzi Mkuu.