Serikali yaendeleza uwezeshaji wajasiriamali Kagera

KAGERA: Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Ajath Fatma Mwasa amekabidhi ofisi, vitendea kazi na usafiri kwa Shirikisho la Umoja wa Wachinga Kagera (SHIUMA) na kuwaahidi serikali itaendelea kuweka mazingira bora biashara kwa wafanyabiashara.
Akizugumza na makundi 20 ya wafanyabiashara ndogo ndogo wapatao 1,600, RC Mwasa alisema hakuridhishwa kuona wafanyabiashara wengi wanapanga bidhaa chini na mbogamboga pembezoni mwa mji jambo ambalo lilimpelekea kukaa na wadau na viongozi mbalimbali wa Manispaa ya Bukoba kuona ni namna wanawezaje kutatua changamoto hiyo.
Alisema jambo lingine alilolibaini kuwa uongozi ambao unawashughulikia wafanyabiashara hao na Machinga haukuwa na ofisi wala vitendea kazi jambo ambalo alilifanyia kazi haraka na sasa ofisi yao ya kutoa huduma na kuwasilisha malalamiko yao, utunzaji wa nyaraka usafiri na vitendea kazi tayari imekamilika kwa matumizi.
Alisema kuwa baada ya kuona changamoto ilivyokubwa ya wafanyabiashara kwa mji wa Bukoba ya kukosa maeneo ya biashara tayari serikali imeridhi kutenga bilioni 10.5 kwa ajili ya jengo kubwa maarufu kama Machinga Complex kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo wote wa mji wa Bukoba na hakuna atakaye kumbana na changamoto ya mvua kali na jua kali mara baada ya jengo hilo kukamilika.
Akitaja faida za wafanyabiashara kufanyia biashara kwenye maeneo mazuri alisema kuwa kwanza ni kukopesheka kirahisi, kuwa na vigezo vya kupata lesseni kutambuliwa na kuchangia maendeleo ya mji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Alito wito kwa viongozi wa SHIUMA kutunza ofisi hiyo na kuitumia kwa maslahi yaliyokusudiwa huku akiwaahaidi wafanyabiashara hao wadogo kuwa serikali itaendelea kuwapa mitaji ,mikopo midogo kuwaunganisha na mifumo ya elimu za biashara mpaka watakapokua na kuwa wafanyabiashara wakubwa
“Swala la ofisi limetatuliwa, tumelimaza sasa kuna eneo la kutunzia nyaraka na kupokea malalamiko ili yaweze kufika serikalini, pia tumewapa usafiri ili mkitaka kwenda kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mkuu wa Wilaya iwe rahisi kufika huko kwa haraka,”.
Kwa upande wake Katibu wa SHIUMA Mkoa wa Kagera, Husna Mohamed alisema kuwa hadi sasa wafanyabiasha ndogo waliojiunga na chama hicho wameongezeka kutoka 3069 hadi kufikia 100,000
Alisema mpaka Juni, 2025, Mkoa wa Kagera umetoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo 200,000 kwa ajili ya kukuza biashara zao ambapo umoja huo umeipongeza serikali kwa kuja na wazo la ujenzi wa eneo la wafanya biashara ndogo kufanyia biashara ambalo litapunguza kero.
Katibu huyo ametoa wito kwa serikali kuendelea kupambana na taasisi za mikopo ya kausha damu ambayo imekuwa chanzo cha kufilisi wafanyabiashara wengi pamoja na baadhi ya viongozi kupunguza masharti katika swala la kutoa mikopo hasa ya asilimia 10.
Uwepo wa wafanyabiashara wengi wanaopanga bidhaa zao chini umekuwa moja ya changamoto inayounyima mkoa wa Kagera fursa ya kukusanya mapato ya ndani ya kutosha kwenye halmashauri za wilaya.