Norway, taasisi kuimarisha thamani ya soya

DAR ES SALAAM: Ubalozi wa Norway nchini Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Private Agricultural Sector Support (PASS) Trust wamesaini makubaliano ya kutekeleza Mradi wa Kuimarisha Mnyororo wa Thamani wa Soya, unaolenga kuendeleza sekta ya kilimo nchini kupitia ubunifu, fedha jumuishi na teknolojia rafiki kwa mazingira.

Kupitia mradi huo, Norway imetoa msaada wa Dola milioni 2.4 huku PASS Trust ikichangia kupitia mfumo wake wa dhamana ya mikopo. Mradi huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakulima12,500, ambapo angalau asilimia 40 watakuwa wanawake na vijana, kwa kuwapatia mbegu bora, teknolojia za kisasa, masoko na huduma za kifedha.

Hadi kufikia mwaka 2028, mradi huo unatarajiwa kuongeza mara tatu uzalishaji wa zao la soya, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuongeza uwezo wa usindikaji wa ndani, hivyo kuboresha uchumi na maisha ya wananchi vijijini.

Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa makubaliano hayo, Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Norway, Kjetil Schie, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya pande zote mbili kukuza kilimo endelevu na jumuishi, sambamba na kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa soya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Trust, Yohane Kaduma, alisema makubaliano hayo yanaashiria dira ya pamoja ya kukuza kilimo chenye tija, kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi na kukuza ajira kupitia sekta ya soya.

Mradi huu unaonyesha uhusiano imara kati ya Tanzania na Norway katika kukuza maendeleo endelevu ya kilimo, usalama wa chakula na ustawi wa wananchi vijijini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button