Pomonda: Jiwe lenye sahihi ya Dk Livingstone Ziwa Nyasa

KAMA kuna eneo adimu lenye historia, uzuri wa asili na ushawishi wa kipekee katika Ziwa Nyasa, basi ni Jiwe la Pomonda.

Jiwe hili lenye ukubwa wa takribani robo hekari, lipo umbali wa meta 250 kutoka Bandari ya Liuli mkoani Ruvuma. Kwa macho ya kawaida, Pomonda ni mwamba tu unaochomoza majini.

Hata hivyo, kwa wenye uelewa wa kina, Pomonda ni hazina ya kihistoria, kijiografia na kiutalii ambayo Tanzania haijaitumia ipasavyo.

Historia inayoishi juu ya maji

Miongoni mwa vivutio vya pekee vya Pomonda ni historia yake. Wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia (1914–1918) na Vita ya Pili ya Dunia (1939–1945), askari wa Kijerumani na Waingereza walitumia mapango ya jiwe hili kama maficho.

Inaelezwa na vyanzo mbalimbali kuwa, Pango kuu la Pomonda, lenye uwezo wa kubeba watu kati ya 60 hadi 100, lilitumika kama ‘ngome ya siri ya kivita.’ Mwongozaji wa watalii na mmiliki wa Pomonda Raha Camp, Joseph Ndomondo anasema,

“Wajerumani waliliita Jiwe la Pomonda kwa jina la ‘Sphinxhaven’ kutokana na mandhari yake ya ajabu. “Waliliona kama sehemu salama ya kujificha lakini pia kitu cha kustaajabisha kwa asili.”

Kwa mujibu Padri mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma, Silivester Mpangala inasemekana kuwa mvumbuzi maarufu wa dunia, Dk David Livingstone aliwahi kutia nanga katika jiwe hilo na kuacha alama au sahihi yake kwenye jiwe hilo.

Dk Livingstone aliyezaliwa mwaka 1813 huko Blantyre, Uingereza alifika Afrika kwa mara ya tatu mwaka 1866, akitafuta chanzo cha Mto Nile.

Safari yake ilipitia Mikindani, Ruvuma, Ziwa Nyasa, Banguela hadi Mweru.

Kwa wakazi wa Liuli, hadithi ya Dk Livingstone ni sehemu ya utambulisho wao na hata milima inayozunguka Mwambao mwa Ziwa Nyasa imepewa jina la Milima ya Livingstone.

Taa ya mataifa matatu

Uchunguzi wa kihistoria umebaini kuwa, kilele cha jiwe hilo chenye urefu wa takribani meta 40, kilikuwa na taa kubwa nyekundu iliyowekwa na wakoloni. Taa hiyo ilikuwa alama ya kuongozea meli katika Ziwa Nyasa na ilitumiwa na nchi tatu za Tanzania, Malawi na Msumbiji.

Hadi leo, mabaki ya nguzo ya taa hiyo bado yanaonekana katika Jiwe la Pomonda, yakikumbusha enzi za usafiri wa maji kwa meli ndogo na za kibiashara zilizotia nanga Liuli. “Taa ile ilikuwa mwanga wa matumaini na urafiki wa mataifa,” anasema Ndomondo

Aliongeza: “Ilitazamwa hata kutoka mbali, pengine hadi upande wa Malawi.” Maumbile ya asili yaliyojaa miujiza Kivutio kingine cha Pomonda ni mawe matatu makubwa yaliyopangwa kwa mpangilio wa kipekee.

Wakazi wa eneo hilo wanaamini Mungu mwenyewe ndiye aliyeyapanga. Mpangilio wake unaruhusu mtumbwi au boti kupita Katikati, jambo linalowashangaza wageni. Kwa macho ya mtaalamu wa jiolojia, ni ushahidi wa nguvu za maumbile; kwa macho ya mtalii, ni muujiza wa uumbaji.

Jiwe la Pomonda pia ni peponi kwa wapenzi wa michezo ya maji.

Hapo unaweza kupiga mbizi, kuruka kutoka kwenye jiwe hadi majini umbali wa meta 30 au kuogelea ukiwa umezungukwa na mandhari tulivu ya ziwa lenye kina cha meta zaidi ya 700. Ndomondo anasema, “Watalii kutoka Ujerumani, Uingereza na Afrika Kusini huja mara kwa mara. Wengi wao husikia kana kwamba wako Bahamas lakini ni Ziwa Nyasa.”

Padri Mpangala anasema madaktari kutoka Uingereza wanafika Liuli kila mwezi kufanya utalii wa tiba katika Hospitali ya Misheni ya Mtakatifu Ana ya Liuli iliyoanzishwa rasmi mwaka 1906, jirani na jiwe hilo. Kwa sasa, baada ya eneo hilo kujaa maji, hospitali hiyo imehamishiwa um- bali wa meta 400 kutoka Ziwa Nyasa.

Makazi ya Samaki wa Mapambo

Kwa mujibu wa utafiti wa wana- sayansi wa mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), eneo linalozunguka Pomonda lina aina zaidi ya 400 za samaki wa mapambo. Samaki hawa hupatikana tu katika maziwa machache duniani.

Hii inafanya Pomonda kuwa ‘paradiso ya wapenzi wa uvuvi wa kiutalii.’ Watalii hupewa fursa ya kuvua samaki hao kwa njia rafiki kwa mazingira, kisha kufurahia ugali wa muhogo unaopikwa na wenyeji wa Liuli; chakula halisi cha Mwambao wa Nyasa.

Pango lenye ukarimu wa asili

Pango kuu la Pomonda ni kivutio cha kipekee. Linatoa kivuli cha asili wakati wa jua kali na hifadhi ya mvua wakati wa masika. Ni mahali bora kwa shughuli za mandari, sherehe ndogo au kupiga picha za ukumbusho.

Hewa safi ya ziwa, mawimbi madogo yanayogonga mawe na mandhari ya Milima ya Livingstone kwa mbali, hutoa hisia ya amani isiyoelezeka.

Ruvuma imebahatika kuwa na utalii wa kiikolojia na kitamaduni.

“Tuna fukwe, visiwa, mapango, Milima ya Livingstone, ngoma za asili na vyakula vya kipekee. Tukivitumia vyema, Ruvuma inaweza kuwa Zanzi- bar ya Kusini.” Mhifadhi na Mbunge mstaafu wa Mbinga, Ngwatura Ndunguru anapongeza uboreshaji wa miundom- binu unaendelea kufanywa na serikali ili kuifungua sekta ya utalii.

Anasema maendeleo ya utalii haya- tawezekana bila uwekezaji kwenye ma- wasiliano, barabara na hoteli za kisasa.

Mwito wa uwekezaji na uhama- sishaji

Martin Ndomba wa Ntembo Tours anashauri Wizara ya Maliasili na Utalii kutuma wataalamu zaidi kufanya utafiti wa kitaalamu katika jiwe hilo. “Pomonda inaweza kuwa kivutio cha dunia kama Serengeti, tukikiendeleza na kukitangaza ipasavyo. Hata ‘documentary’ makala) za kimataifa zinaweza kupigwa hapa,” anasisitiza Ndomba.

Ni ukweli unaouma kwamba, Watanzania wengi wanapendelea kutazama vivutio vya nje, wakati hazina za kipekee kama Pomonda zipo nyumbani. Elimu ya utalii inapaswa kuanza shuleni na kampuni za ndani zipewe motisha kutangaza vivutio vya Mikoa ya Kusini.

Almasi inayosubiria kung’aa

Jiwe la Pomonda si tu kipande cha mwamba ndani ya Ziwa Nyasa, ni nyaraka ya historia ya ukoloni, alama ya utafiti wa Dk Livingstone, makazi ya samaki wa mapambo na jukwaa la utalii wa maji. Wakati huu wa kuvumbua utalii wa ndani, Pomonda inapaswa kuangaziwa kama ‘almasi iliyosahaulika’ ya Tanza- nia.

Kama watalii wa ndani wataanza kuliona jiwe hili kwa macho ya fursa na serikali ikawekeza katika miundombinu, basi Pomonda itakuwa kivutio cha matumaini mapya ya utalii wa Kusini.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button