ZEC : Maandalizi ya uchaguzi yakamilika

TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imesema maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo yamefikia hatua nzuri, ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa uchapaji na upokeaji wa karatasi za kura.

Akizungumza na HabariLEO , Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina amesema tume imepokea karatasi za kura 717,557, hatua inayothibitisha ukamilifu wa maandalizi na utayari wa tume kwa uchaguzi. “Kupokelewa kwa karatasi hizi ni ishara kuwa tumefikia hatua ya mwisho ya maandalizi ya vifaa vya uchaguzi. Tunajivunia kwamba kila kitu kimekamilika kwa wakati,” alisema.

Alifafanua kuwa uchapaji wa karatasi hizo ulifanyika kwa mara ya kwanza ndani ya Zanzibar kupitia Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar (ZGP), baada ya mchakato wa zabuni ulioshirikisha kampuni nne kutoka Afrika Kusini, China na Zanzibar. SOMA: ZEC yawateua wagombea 11 Urais Zanzibar

Kwa mujibu wa Faina, hatua hiyo ni ya kihistoria kwani ni mara ya kwanza kwa Zanzibar kuchapisha karatasi za kura ndani ya nchi, jambo ambalo limefanikiwa katika mataifa machache Afrika. “Huu ni wakati wa fahari kwa Zanzibar. Tumethibitisha uwezo wetu wa ndani wa kuzalisha nyaraka zenye viwango vya juu vya usalama,” alisema.

ZEC imesema uchapaji huo uligharimu Sh milioni 908.3 pekee, kiwango kilicho chini ya bajeti ya awali ya Sh bilioni 1.24, hivyo kuiwezesha serikali kuokoa zaidi ya Sh milioni 300 bila kuathiri ubora wa kazi.
Faina alisema ZGP ilikamilisha kazi hiyo kabla ya muda uliopangwa, jambo linaloonesha uwajibikaji na weledi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha, alibainisha kuwa vifaa vyote vya uchaguzi vimeshasambazwa katika ofisi za wilaya, huku karatasi za kura zikitarajiwa kupelekwa kwenye vituo kwa mujibu wa ratiba rasmi ya tume. Wawakilishi wa vyama vya siasa waliotoa maoni yao wamesifu uwazi wa ZEC na ushirikishwaji wa wadau wote katika maandalizi hayo, wakisema hatua hiyo imeongeza imani kwa mchakato mzima wa uchaguzi.

Faina alisema ZEC inaendelea kushirikiana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika. ZEC inasimamia uchaguzi wa urais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani, wakati INEC inasimamia uchaguzi wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wabunge wa Bunge la Muungano.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button