Kiswaga ahitimisha kampeni kwa kishindo na ahadi kubwa za maendeleo

IRINGA: Moshi wa kisiasa umetanda Jimbo la Kalenga baada ya mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jackson Kiswaga, kufunga kampeni zake kwa kishindo kikubwa leo Jumapili, Oktoba 26, katika viwanja vya Zahanati ya Magulilwa, huku maelfu ya wananchi wakimiminika kumpokea kwa hamasa na matumaini mapya ya maendeleo.

Baada ya siku 42 za kampeni zilizopambwa na mikutano mikubwa katika kila kata na kijiji, Kiswaga aliwasili Magulilwa akihitimisha safari ya kisiasa iliyowagusa wananchi wa kila kona ya Kalenga.

Shughuli hiyo ya kufunga pazia la kampeni iligeuka kuwa sherehe ya kijamii na kisiasa, huku wananchi wakiahidi kwa sauti moja kumpa kura za kishindo ifikapo Oktoba 29, siku ya uchaguzi mkuu.

Katika mkutano huo wa kihistoria, uliohudhuriwa na wagombea wote wa udiwani wa CCM katika Jimbo la Kalenga akiwemo mwenyeji Boazi Mbilinyi, viongozi wa chama, wazee wa kimila, na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Ndugu Constatino Kihwele – ambaye alikuwa mgeni rasmi – walisifu kazi kubwa iliyofanywa na Kiswaga katika muhula wake wa kwanza, wakimtaja kuwa “nguvu ya maendeleo ya Kalenga.”

Akizungumza kwa hisia na msisitizo mkubwa, Kiswaga aliwaomba wananchi wampe ridhaa ya pili ili aendelee kusukuma mbele gurudumu la maendeleo lililoanza kusonga kwa kasi chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

“Tumeona miradi ya maji, shule mpya, zahanati, barabara na umeme. Kalenga inabadilika! Lakini safari bado haijaisha — tuendelee na CCM, tuendelee na Samia, tuendelee na kazi,” alisema Kiswaga huku wananchi wakishangilia, “Kiswaga! Kiswaga! 2025!”

Kiswaga alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka historia kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini, na kwamba utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025–2030 utakuwa ni mwendelezo wa kasi ya mabadiliko hayo.

Akiwaomba wananchi wa Kalenga wamchague tena kuwa mbunge wao, Kiswaga aliahidi kusimamia kwa karibu miradi yote aliyoianzisha katika kipindi chake cha kwanza (2020–2025), ikiwemo miradi ya maji, umeme, kilimo, elimu, afya na barabara, akisema safari ya maendeleo ya Kalenga “bado inaendelea, haijakamilika.”

“Kalenga ni nyumbani kwangu, na nitapigania kila kijiji, kila mtoto, na kila mwananchi apate maendeleo. Tukiendelea kushikamana chini ya CCM, hakuna litakaloshindikana,” alisema Kiswaga kwa msisitizo mkubwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button