SWAUTA yapongeza Ilani CCM

TAASISI ya Sauti ya Wanawake Wenye Ulemavu Tanzania (SWAUTA) imekipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuonesha kuwajali watu wenye ulemavu kwa kuandika ilani ya uchaguzi kwa maandishi ya wasioona (nukta nundu).
Swauta imesema inaamini mambo aliyoahidi mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho, Samia Suluhu Hassan kuhusu maandalizi ya katiba mpya, atayatekeleza. Akizungumza na HabariLeo Mkurugenzi wa Swauta, Stella Jailos amesema mwenendo wa kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu.
Jailos alisema ahadi na hatua hiyo ya CCM ni mwanzo mwema unaopaswa kuigwa na vyama vingine kwa kulijali kundi la Watanzania wenye ulemavu. “Tunaamini wenye ulemavu watashirikishwa kwenye jopo litakaloundwa kushughulikia katiba mpya hususani wanawake wenye ulemavu na hata katika mchakato wa ajira mpya baada ya uchaguzi,” alisema.
Amesema kwa mtazamo wake, CCM kimekuwa chama mwalimu kwa vyama vingine kwa kuwa ndicho pia chama cha siasa cha kwanza nchini kufikiria nafasi za ubunge kwa kundi la wanawake wenye ulemavu. “Sasa kimekuwa chama cha kwanza pia kuandika ilani ya uchaguzi kwa maandishi ya wasioona na maandishi makubwa kwa ajili ya watu wenye ualbino na wenye uoni hafifu,” alisema Jailos.
Akaongeza: “Hili ni jambo jema maana hata tusioona siku yoyote tukitaka kuhoji kuhusu jambo fulani ambalo halijatekelezwa, tutarejea kwenye ilani hiyo…” Kwa mujibu wa Jailos, ingawa nakala 500 ni chache, ni hatua na mwanzo mzuri wa kuigwa na kupongeza. “CCM ni chama cha kwanza katika nchi hii kufikiria na kukumbuka kuwa kuna kundi la watu wasioona na watu wenye uoni hafifu wanaotakiwa pia kujua yaliyo kwenye ilani za vyama,” alisema.
Hatahivyo ametoa wito kwa vyama vyote vya siasa kuzingatia na kuiga yaliyofanywa na CCM ili watu wasioona wasome na kujua yaliyo katika ilani za vyama mbalimbali ili hata wanapozungumzia ahadi za vyama hivyo, wazungumze kwa rejea na kutoa hukumu ya haki. SOMA: Taasisi yasisitiza kulinda bunifu mpya
Jailos alisema: “Hatua hiyo itatufikisha mbali kidemokrasia na kijamii”. Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo wa Swauta, hata baada ya uchaguzi wa mwaka huu, vyama vijiandae kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi zinazofuata ikiwa ni pamoja na kuwajengea mazingira rafiki na kuwawezesha kupata nyenzo za uchaguzi na uongozi.



