CUF kuongeza ushindani masoko ya hisa

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema serikali yake itaruhusu masoko mengine ya hisa na mitaji yafanye kazi sambamba na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ili kuongeza ushindani. Ilani ya uchaguzi ya CUF 2025-2030 imeeleza hatua hiyo itatoa uwanja mpana zaidi wa wanunuzi na wauzaji wa hisa kuchagua.
Chama kimeahidi kuimarisha soko la mitaji kama sekta yenye nguvu ya kugharamia uzalishaji wa kampuni katika sekta za kilimo, viwanda, biashara na huduma yenye uwazi na ushiriki wa wananchi wote wenye akiba za kuwekeza.
CUF imeahidi kuimarisha DSE na itahamasisha kampuni zaidi yenye sifa kujiorodhesha kwenye soko la hisa. Ilani imeeleza serikali ya CUF itaruhusu kampuni mpya zinazosajiliwa kujiorodhesha DSE kwa utaratibu maalumu ili ziweze kuuza hisa zake kukuza mitaji yao. Pia, CUF imeahidi kuhamasisha kampuni na mashirika ya serikali yaliyobinafsishwa kujiorodhesha DSE. SOMA: CUF yahimiza kupiga kura Oktoba 29
“Itaimarisha teknolojia na uwezo wa kushiriki kwenye masoko ya hisa kwa kuboresha ‘Hisa Kiganjani’ ipatikane kwa urahisi kwa lugha ya kiswahili na kiingereza.Iweze kutoa elimu na taarifa fupi kuhususoko la hisa na matangazo ya hisa mpya (IPO) kupitia simu,” imeeleza ilani.
CUF imeahidi kuliunganisha soko la hisa na mitandao ya malipo ya simu kurahisisha malipo na mapato ya hisa kwa washiriki wa soko la hisa. “Itaimarisha kanuni zinazoyataka makampuni kuweka mahesabu sahihi na pia itaimarisha huduma za ukaguzi,” imeeleza ilani.



