Wagombea urais wataka 4R iwe sheria

WALIOKUWA wagombea wa nafasi ya urais kwa tiketi za vyama vya siasa vya upinzani wameshauri falsafa ya 4R ipitishwe na bunge ili iwe sheria ya kudumu itakayotekelezwa na vyama vyote vya siasa. Wagombea hao ni kutoka Chama cha Democratic (DP), Chama cha MAKINI, Alliance for African Farmers (AAFP), Chama cha Sauti ya Umma (SAU) pamoja na Chama cha Tanzania Labour (TLP).

Dhana ya falsafa ya 4R inabeba Maridhiano; ikimaanisha kukaa chini na kuzungumza juu ya jambo fulani, Ustahimilivu ikimaanisha kuvumiliana katika kila hali, Mabadiliko ikilenga kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na mwisho ni Kujenga upya ikihusisha kusahau yaliyopita na kuanza upya.

Akizungumza na HabariLEO, aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya DP, Abdul Mluya alisema falsafa ya 4R kuwa ajenda ya kitaifa ni sawa na ipitishwe bungeni kama sheria ili kila chama kitakachoingia madarakani kiitekeleze. “Suala hili la 4R niliwahi kulizungumza, liingizwe kwenye ajenda za kitaifa ili liweze kupitishwa na bunge na iwe moja ya dira ya taifa,” alieleza.

“Halitakiwi kubaki kwa rais na pale anapomaliza muda wake linaishia hapo, bali linatakiwa kuwa ni ajenda ya kitaifa ya kudumu na rais yeyote ajaye madarakani, hata kama anatokea chama pinzani, anapopewa ridhaa ya kuongoza ni lazima azitekeleze falsafa hizo,” alisema Mluya.

Coaster Kibonde aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya Chama cha MAKINI, alisema falsafa ya 4R kuwa ajenda ni suala muhimu na kila mtu anatakiwa kuliishi na aliyelianzisha akawe kinara wa kuzitekeleza kwa sababu kwa kufanya hivyo kutasaidia kuondoa changamoto mbalimbali. Alisema utekelezaji wa falsafa hiyo utasaidia kuondoa viongozi wenye uchu wa madaraka, kuwajibishwa na kusaidia kupatikana viongozi watakaowatumikia wananchi na si kukimbilia Ikulu.

Kuhusu nini kifanyike ili Tanzania iendelee kuwa na amani, umoja na utulivu, aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya SAU, Majalio Kyara alisema ni wakati wa serikali kukaa chini na wadau kujadili na kupokea maoni ili kujua wapi wamekosea, kurekebisha na kuanza upya.

Alisema jambo lililotokea linaonesha kuna shida mahali japo halikuleta majawabu yaliyotakiwa zaidi limeacha maumivu kwa wananchi. “Jambo la hekima na busara na kurejesha amani yetu ni kukaa chini kuzungumza, kujua makosa yako wapi au ni akina nani wamekosea, kufungua ukurasa wa maoni kwa wadau ili waseme nini kifanyike, kwa sababu hasara ni kubwa kwa nchi na jamii kwa ujumla,” alisema.

Aliongeza: “Na jambo muhimu la kutambua ni kuwa tunategemewa na nchi nyingi kupitia bandari, hivyo wadau wakikutana na kujadili hili ni wazi watakuja na majibu yatakayoponya majeraha.” Aidha, Kyara alizitaka taasisi za dini kufanya maombi kwa ajili ya taifa.

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya AAFP, Kunje Ngombale Mwiru alisema ni muhimu serikali ikaanzisha madarasa ya kufundisha vijana uzalendo yatakayosimamiwa na wastaafu waliowahi kufanya kazi enzi za Baba wa Taifa, Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, na Benjamin Mkapa ili wajue wapi nchi imetoka na inakotakiwa kwenda. “Kuna watu wana wivu na amani tuliyonayo. Ni wakati wa kusafisha nchi kwa kujua idadi ya watu wangu, kwa sababu taifa letu limekumbwa na watu ambao ni kutoka nje ya nchi na hawana vibali.

Hivyo basi Uhamiaji na wote wanaosimamia mipaka wapewe mbinu mpya za namna ya kuzuia watu hao, kwa sababu wanapoingia mitaani wanaleta tabia ambazo si nzuri,” alisema. Kuhusu nini serikali ifanye ili kulinda amani, wote walisema mshindi apitie ilani za vyama vyote na kuzifanyia kazi kwa kuyatekeleza matakwa ya wananchi kupitia rasilimali za nchi. Mgombea wa urais kwa tiketi ya TLP, Rwamugira Yustas alisema kila kiongozi aliyechaguliwa awe mzalendo kwa kuwatumikia wananchi.

“Wito wangu kwa viongozi wote wa vyama vya siasa, tusiwalishe maneno machafu wafuasi wetu, kwa sababu maneno hayo yanaishi na yanafanyiwa kazi hata baada ya wewe uliyetamka kufa au kuacha siasa, na mwisho matokeo yake yanakuwa kama kilichotokea Oktoba 29 mwaka huu,” alisema Mgombea wa Chama cha MAKINI, Coaster Kibonde.

Alisema suala la kulinda amani ni jukumu la kila mmoja, lakini Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ina jukumu la kuzuia maudhui yanayosambazwa mitandaoni, yakiwa na lengo la kuchochea vurugu kabla hayajafika kwa jamii na kuleta maafa makubwa. SOMA: Vijana watakiwa kuepuka mihemko na kulinda amani uchaguzi mkuu

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button