Bunge lamthibitisha Mwigulu

BUNGE limethibitisha Mbunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba awe Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wabunge wamemthibitisha Dk Mwigulu kwa kura za ndiyo 369 kati ya kura 371 zilizopigwa bungeni jijini Dodoma jana. Dk Mwigulu anamrithi Kassim Majaliwa ambaye ameshikilia wadhifa huo kwa miaka 10 sasa, akianzia Serikali ya Awamu ya Tano na awamu ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Watanzania wengine waliowahi kushika wadhifa huo ni Julius Nyerere, Rashidi Kawawa, Edward Sokoine, Joseph Warioba, Salim Ahmed Salim, John Malecela, Cleopa Msuya, Frederick Sumaye, Mizengo Pinda na Edward Lowassa.
Saa 3:05, Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alimruhusu Mpambe wa Kijeshi wa Rais, Brigedia Jenerali, Nyamburi Mashauri aingie bungeni. Saa 3:07, Brigendia Jenerali Mashauri alimkabidhi Spika Zungu bahasha iliyokuwa na ujumbe maalumu. “Nimeelekezwa na Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan na Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha ujumbe maalumu kwako,” alisema na kukabidhi bahasha hiyo.
Zungu alisoma ujumbe huo akisema: “Hivyo kwa kutekeleza matakwa ya Katiba ibara ya 51(2), nimemteua Dk Lameck Mwigulu Nchemba Mbunge, ili uteuzi wake uthibitishwe na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari aliliomba Bunge lithibitishe uteuzi wa Waziri Mkuu uliyofanywa na Rais kwa mujibu wa Ibara ya 51 (2) ya Katiba inayoelekeza kufanya hivyo ndani ya siku 14 tangu Rais kushika madaraka. SOMA: Dk Mwigulu apokelewa Ofisi ya Waziri Mkuu
Johari alisema majukumu ya Waziri Mkuu kama yalivyoelezwa na Ibara ya 52 ya Katiba atakuwa na madaraka ya juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku kwa siku wa kazi na shughuli za serikali. Alisema pia Waziri Mkuu atakuwa kiongozi wa shughuli za serikali bungeni na atakuwa na madaraka ya kutekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo au mambo yoyote ambayo rais ataagiza yatekelezwe.
“Waziri Mkuu ni kiungo muhimu kati ya Bunge na serikali na kwa maneno mengine, yeye ni daraja muhimu kati ya wananchi na serikali na ni msaidizi mkuu wa rais katika kutekeleza majukumu yake,” alisema Johari.
Amesema majukumu mazito na makubwa yanamuhitaji mtu ambaye ni mchapakazi, hodari, anayejituma, mwenye busara na upeo mpana wa uelewa wa mambo. Johari alisema pia awe mwenye uwezo wa kubeba majukumu mengi bila ya kutetereka na kuongeza kuwa, madaraka hayo yanamuhitaji mtu makini katika kulinda na kutetea katiba, sheria, kanuni na taratibu. “Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amewasilisha jina la Dk Lameck Mwigulu Nchemba ili athibitishwe na Bunge na ana sifa,” alisema Johari.
Aliongeza: “Dk Mwigulu si mgeni kwa waheshimiwa wabunge lakini si mgeni kwa wananchi, historia yake katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kuwa nazo inalithibitisha hili. Watu wengi pamoja na wabunge wanaufahamu uwezo wake wa kufanya kazi, uwezo wa kufanya kazi usiku na mchana bila ulalamishi, uwezo ambao umejidhirisha muda wote alioshika nyadhifa za uongozi wa umma ndani ya serikali na katika taifa kwa ujumla”.



