Mwigulu: Nakuja na fyekeo

WAZIRI Mkuu mteule, Dk Mwigulu Nchemba ameonya watumishi wa umma wavivu, wazembe na wala rushwa. Dk Mwigulu ameagiza waache mara moja kwa sababu anakuja na fyekeo na rato kusafisha uovu katika ofisi zao.
Amesema hayo bungeni Dodoma jana wakati akishukuru wabunge kwa kumthibitisha awe Waziri Mkuu. Dk Mwigulu aliwataka watumishi wa umma na Watanzania kwa ujumla wawe tayari kwenda kwa gia ya kupandia mlima, ya kupita katika bahari yenye mawimbi na ya kupita kwenye anga lenye mawingu.
“Kwa watumishi wa umma wavivu, wazembe, wala rushwa na wenye lugha mbaya kwa Watanzania ndani ya ofisi za umma tuwe tayari, nitakuja na fyekeo na rato. Lazima maono na ahadi ambazo Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) alizotoa kwa Watanzania zitekelezwe,” alisema.
Dk Mwigulu amehakikishia Watanzania, hususani wanyonge watasikilizwa katika kila ofisi ya umma.“Kila aliye Mtanzania, hii nchi ni yake. Watanzania wote watasikilizwa kwa nidhamu katika ofisi za umma. Watafikisha kero zao na watumishi wa umma watakwenda kwenye maeneo ya wananchi kutatua kero za Watanzania,” alisema.
Dk Mwigulu ametoa rai kwa Watanzania wote kumtanguliza Mungu mbele ili taifa liweze kuwa na amani na utulivu, kusudi yale yote aliyoahidi Rais Samia na Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi yaliyopo kwenye ilani na yaliyoahidiwa na wabunge yatimizwe vizuri.
Amejivunia mafanikio ya utendaji wa Rais Samia kwamba amejitambulisha kama mtatuzi wa changamoto za Watanzania kutokana na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Mathalani, alisema Rais Samia ameweza kumaliza changamoto ya mgao wa umeme uliokuwa unalitesa taifa kutokana na kukamilisha mradi mkubwa wa Bwawa la Kuzalisha Umeme wa Maji la Julius Nyerere na sasa nchi ina umeme wa ziada.
Mbali na hilo, alisema Rais Samia amefanikiwa kupunguza vifo vya mama na mtoto kutokana na kujenga na kukamilisha hospitali zaidi ya 119 za wilaya, vituo vya afya zaidi ya 649 na zahanati zaidi ya 2,800 nchi nzima. Dk Mwigulu alisema Rais Samia amepunguza uhaba wa shule na madarasa katika sekta ya elimu ambapo kwa kipindi kifupi amejenga shule za msingi zaidi ya 2,700, shule za sekondari zaidi ya 1,300 na madarasa zaidi ya 97,000.
Ameahidi kufanya kazi kwa bidii, weledi na uaminifu na kwa jitihada ili kukidhi matarajio ya Rais Samia. Dk Mwigulu ameahidi kumpa ushirikiano Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu ili aweze kutekeleza ahadi yake ya kulifanya Bunge la 13 kuwa la Watanzania. Vilevile, aliwaahidi wabunge kuwa serikali itashirikiana na kupokea maoni yao na kwamba itafanya hivyo bila ubaguzi wowote na kwamba hata wabunge wachache watapewa fursa sawa.
Amemshukuru Rais Samia kwa imani kubwa aliyonayo kwake hadi kumpendekeza kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania. “Natambua uzito wa majukumu haya pamoja na matarajio yake na Watanzania na nitafanya kazi kwa bidii, kwa uaminifu kukidhi matarajio hayo,” alisema Dk Mwigulu.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeanzisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 na kipindi cha pili cha Awamu ya Sita kinaanza kuitekeleza dira hiyo. Ameongeza kuwa, dira hiyo imebeba matumaini makubwa ya vijana ambao ndio haswa walengwa wa dira husika na kusisitiza serikali ina kazi kubwa ya kuanza vizuri utekelezaji, huku ikimalizia viporo vya dira iliyopita.
Amesema serikali itaratibu mpango mkakati wa kutengeneza ajira za vijana milioni nane kwa kushirikiana na sekta binafsi, ikiwa ni ahadi ya Rais Samia kwa vijana. “Pamoja na Tanzania kuwa nchi tajiri, bado kuna asilimia zisizopungua nane za Watanzania wanaoishi katika umasikini wa kupindukia.
Tuna takribani asilimia 26 ya wananchi wanaoishi katika umasikini wa kipato,” alisema Dk Nchemba. Alisema anaufahamu na kuuishi umasikini wa Watanzania na si kuusoma katika kitabu na kwamba miaka 32 ameishi katika maisha ya umasikini. SOMA: Bunge lamthibitisha Mwigulu
Pia ameeleza namna alivyoishi na kukulia katika umasikini ambapo wakati fulani alitumia nguo ambayo dada yake alikuwa akijifunga kiunoni kwa ajili ya kujifunika usiku. Amesema anatambua ugumu wa maisha hayo, huku akitolea mfano mazingira ya ufugaji ambapo akitoka kuchunga mifugo aliingia katika nyumba inayovuja wakati wa mvua, hali iliyomfanya kujifunika ngozi ili kujikinga na matone ya mvua.



