TRA kulinda biashara binafsi

DAR ES SALAAM: KAMISHNA Mkuu  wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amesema mamlaka hiyo itashirikiana na wafanyabiashara kulinda biashara zao binafsi ili ziendelee kukua.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana alipowatembelea wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo kutoa pole kwa changamoto zilizotokea na kuangalia hali ya biashara kwa sasa, Mwenda ametoa wito kwa wanunuzi wote ambao wanategemea soko hilo na sehemu zingine kuwa  biashara zinaendelea vizuri.

“Nimekuja kuona shughuli wanazofanya lakini pia kuwapa pole kwa changamoto zilizotokea kuna baadhi hawajafungua biashara nimekuja kuona biashara zinaendeleaje na nimefurahi kuona biashara zinaendelea kama kawaida na nimethibitishiwa na nilioongea nao wanauza kama kawaida na wateja wanakuja,”amesisitiza Mwenda.

Aidha, amewathibitishia uongozi kwa niaba ya wafanyabiashara binafsi kwamba biashara hiyo ni ya umma kwani  wakiwa wanafanya shughuli zao umma unafaidika na huduma, kodi inayopatikana, kwa wengine kufanya manunuzi.

“Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu wakati anafanya kampeni alisema Tume ya Rais ya Kurekebisha Masuala ya Kodi imekamilisha kazi na serikali ikishaundwa itatoa ripoti yake .Moja ya changamoto walizozungumzia ni masuala ya kisera nimewathibitishia kwamba pindi ripoti itakapotoka TRA itashirikiana nao kuhakikisha yale mapendekezo ya kutatua changamoto za muda mrefu zitatekelezwa na kutatuliwa,”amesema.

Amesema wafanyabiashara ni washirika wao hivyo zile changamoto zenye uthibitisho zilizojitokeza watachukua hatua za kuleta unafuu kwao .

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severine Mushi amesema wamefurahi kwa kamishna wa TRA kuwapa pole kwa athari zilizotokea kabla na baada ya uchaguzi hatua hiyo ni kuonesha kujali na amewasikiliza.

“Pamoja na lile sekeseke eneo letu lilibaki salama na sasa biashara zimechangamka zimerudi kawaida tunatarajia kukua kuelekea mwisho wa mwaka. Hasara ni kubwa mtandao ulizimwa hakufanya kazi hivyo biashara za online zilishindikana.

Kuhusu waliopata changamoto binafsi amesema watawasilisha ripoti kwa meneja wa TRA kuhakisha changamoto hizo zinatatuliwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button