Tume Uchunguzi vurugu Oktoba 29 yazinduliwa

RAIS Samia Suluhu Hassan amezindua Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Ameitaka tume hiyo kuchunguza zilipotoka fedha wanazodaiwa kupewa vijana walioandamana na kufanya uhalifu. Rais Samia alisema hayo jana Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma wakati akiizindua na kuipa tume miezi mitatu kukamilisha uchunguzi huo.

Sambamba na hayo, aliitaka tume hiyo kuchunguza madai ya vijana kutaka haki, kwamba ni haki gani waliokosa ili serikali iwapatie. Pia, ameitaka tume kuangalia ushiriki wa taasisi zisizo za serikali (NGO) za ndani na nje ya nchi katika vurugu hizo zilizosababisha maafa makubwa.

Amesema kilichotokea siku ya uchaguzi hakikutarajiwa kutokea ndani ya nchi kwa sababu ya historia ya nchi ya usalama na utulivu wa kisiasa. “Hata kama tuna vipindi tulikuwa hatuna utulivu wa kisiasa lakini hatukufikia kiasi hiki kilichofikia. Tume itakapokabidhiwa makabrasha ya kufanyia kazi, itakabidhiwa na hadidu za rejea watakazokwenda kuziangalia na kuzifanyia kazi,” alisema Rais Samia.

Aidha, ameiagiza tume ikaangalie sababu ya vijana kuingia barabarani na kufanya vurugu na kujua kiini cha tatizo hilo. Amesema vijana waliingia barabarani kudai haki, hivyo tume ije na majibu ni haki gani wanayodai vijana ili serikali iweze kuifanyia kazi kwa haraka na waweze kuipata haki yao. SOMA : Waziri Mkuu akutana na Katibu TEC

Kadhalika, Rais Samia aliitaka tume kwenda kuangalia matamshi ya vyama vya upinzani ambavyo baadhi yao waliahidi kuzuia uchaguzi, hivyo kuja na majibu kuwa ni kitu gani hasa kilisababisha kufanya vile. Rais Samia aliikumbusha tume kuhakikisha katika kuchunguza matamshi ya chama husika, pia iangalie uhusiano wa chama hicho na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ulikuwaje katika kipindi hicho hadi kusababisha kusema maneno hayo.

Ameongeza: “Lingine tuangalie ‘role’ (ushiriki) ya mbali na vyama vya siasa vilivyoingia katika huo mgogoro, tuangalie taasisi zisizo za serikali (NGOs) za ndani na nje ya nchi.Tunaambiwa kwamba vijana waliokuwa wanadai haki walilipwa fedha kwanza, ndio wakaingia barabarani.” Amesema  vijana wengi waliingia barabarani kuendana na fedha walizolipwa, hivyo tume iangalie fedha hizo zimetoka wapi na NGOs hizo zimechangia nini katika viurugu hizo.

Amebainisha kuwa, hata kama kulikuwa na changamoto baina ya INEC na vyama vya siasa, msajili na vyama vya siasa na serikali na vyama vya siasa, je, hakukuwa na njia nyingine nzuri zaidi ya kutatua changamoto hizo kuliko ile iliyoleta vurugu na upotevu wa amani, kuchoma nchi na kusababisha vifo vya wananchi? “Tukaangalie, jambo limetokea watu wameingia barabarani na vurugu zimetokea.

Tuangalie njia zilizochukuliwa kukabiliana na zile vurugu na ndio maana katika tume tuna mstaafu jeshi na mstaafu polisi. Twende tukaangalie njia zilizochukuliwa zilikuwaje,” alisisitiza Rais Samia. Amesisitiza katika kutekeleza jukumu hilo, tume itapewa miezi mitatu na kwamba itawezeshwa vifaa ili itekeleze majukumu yake kwa urahisi. Amesema ili kuisaidia tume, serikali itaipa tume hiyo sekretarieti itakayoisaidia kuandika pamoja na mambo mengine yote yanayotakiwa kufanywa ili iweze kutekeleza wajibu wake vizuri.

“Kama mnavyojua, wakati nazindua kampeni niliahidi kuwa ndani ya siku 100 nitaweka tume ya maridhiano kuangalia changamoto za kisiasa ndani yetu, tupatane na twende vizuri. Lakini kwa hili lililotokea, tumeona tuunde tume kwanza ifanye kazi yake, imalize mapendekezo yatakayotoka huku, ndiyo tutakayoyafanyia kazi kwenye tume ya maridhiano,” alisema. Rais Samia alisema mapendekezo ya tume ya uchunguzi ndiyo yatakayofanywa ajenda kwenye tume ya maridhiano.

Amesema  pamoja na baadhi ya wanasiasa wa upinzani kusema hawana imani na tume ya ndani, yeye binafsi ana matumaini makubwa na tume hiyo kutokana na ubobezi na uzoefu mkubwa walionao wajumbe wa tume hiyo na kwamba anategemea mapendekezo yataisaidia nchi kusonga mbele. Rais Samia alieleza kuwa, uundaji wa tume hiyo umeendana na Sheria ya Tume za Uchunguzi ya Mwaka 2023 sura ya 32 ambayo inampa rais mamlaka ya kuunda tume mbalimbali.

Wakati akizindua Bunge la 13 mjini Dodoma, Rais Samia aliahidi kuunda Tume ya Uchunguzi wa vurugu za siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi. Rais Samia alimteua Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othmani kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo. Jaji Chande ni kiongozi mwenye uzoefu katika tasnia ya sheria, utoaji wa haki na masuala ya haki za binadamu kitaifa na kimataifa.

Anafahamika na kuheshimika kimataifa kutokana na uelewa alionao wa masuala ya sheria na siasa za kimataifa kwenye masuala ya utunzaji wa amani. Wajumbe walioteuliwa na Rais Samia ni pamoja na Jaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Ibrahim Juma aliyekuwa Jaji Mkuu tangu mwaka 2017 hadi alipostaafu mwaka 2025.

Kabla ya kuwa Jaji Mkuu, aliwahi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama Kuu na Profesa wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).Pia, Rais Samia alimteua mwanadiplomasia na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue kuwa mjumbe wa tume hiyo. Akiwa Katibu Mkuu Kiongozi kwa nafasi yake, aliwahi pia kuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri, Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa na Mkuu wa Utumishi wa Umma.

Kama Katibu Mkuu Kiongozi, pia alisimamia kazi za tume ambazo ziliundwa na rais wa wakati huo. Mjumbe mwingine aliyeteuliwa na Rais Samia ni mwanadiplomasia na Balozi mstaafu, Radhia Msuya ambaye alihudumu kama Balozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali, ikiwemo Afrika Kusini, Namibia, Lesotho, Botswana na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Kutokana na weledi wake kazini, Balozi Msuya aliwahi kutunukiwa Nishani ya Heshima ya National Oder of Merit na Rais wa Ufaransa. Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu, Paul Meela ambaye ni Luteni Jenerali mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akiwa kazini, Balozi Meela alishiriki katika shughuli nyingi za kuleta amani Darfur nchini Sudan na alishiriki katika usuluhishi katika timu ya usuluhishi chini ya Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta.Pia, Rais Samia amemteua Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IJP) mstaafu, Said Mwema ambaye katika utumishi wake alifanikisha mageuzi makubwa ndani ya Jeshi la Polisi.

Amefanikiwa kuandaa na kutekeleza mkakati wa polisi jamii na kuliongoza jeshi la polisi kupambana na uhalifu, ukiwemo uhalifu wa kuvuka mipaka, ugaidi, biashara haramu ya binadamu na dawa za kulevya. Wengine ni mwanadiplomasia na Balozi mstaafu, David Kapya ambaye aliwahi kufanya kazi mbalimbali katika utatuzi wa migogoro, ikiwemo kuwa Msaidizi Mahususi wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa katika mazungumzo ya kutafuta amani Mashariki mwa DRC.

Mwingine ni aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk Stergomena Tax ambaye ni kiongozi mwandamizi mstaafu mwenye uzoefu katika masuala ya uongozi, diplomasia na utangamano wa kikanda. Amehudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani na nje ya nchi, ikiwemo nafasi ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Rais Samia azidi kuisuka Wizara ya Maendeleo ya Vijana.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button