Vijana watakiwa kutumia hotuba ya rais kupata suluhu

VIJANA nchini wametakiwa kuijadili na kuitumia hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizindua Bunge la 13 kama suluhu ya changamoto zinazowakabili. Wakizungumza na HabariLEO viongozi wa wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga walisema hotuba ya Rais Samia imeweka msingi wa utatuzi wa changamoto zinazowakabili katika maisha yao.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamachinga Tanzania, Stephen Lusinde alisema kama kuna jambo ambalo vijana wanalitaka walidai jambo hilo kwa njia za kistaarabu kupitia kupeleka ombi la kuonana na Rais Samia ili awasikilize kuliko kuiharibu nchi yao kwa mikono yao wenyewe.

Amesema kila Mtanzania alionja athari ya vurugu za siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi kwa sababu zilizosababisha maisha kuwa ghali kutokana na bidhaa za kawaida kupanda bei. SOMA: Tume Uchunguzi vurugu Oktoba 29 yazinduliwa

Lusinde ambaye pia ni Mwenyekiti wa Machinga, Soko la Kariakoo aliwataka vijana kukataa maandamano katika maisha yao kwani ndio chanzo cha kuyeyusha ndoto za vijana pamoja na kuhatarisha maisha ya watoto ambao ni vijana wa baadaye. “Sote tushiriki kwa vitendo kuilinda nchi yetu, tudumishe umoja na utulivu tuachane na chokochoko za kidini ambazo hazina tija wala faida kwa yeyote zaidi ya kutuletea laana na mikosi katika maisha yetu,” alisema.

Ameongeza  kuwa kila Mtanzania atumie nafasi yake kuilinda nchi na kutoshiriki kuichoma kwa kukataa ushawishi kutoka kwa watu wasioitakia mema nchi kwa maslahi yao binafsi. Lusinde amewataka viongozi wa kisiasa wanaohusika na vurugu na kushawishi watu kuandamana, wasikilize ushauri wa Rais Samia wa kuanzisha mchakato wa maridhiano ili kuiponya nchi.

Ametoa mfano wa athari za vurugu hizo kuwa ni uharibifu wa mali za umma na kuwafanya wananchi wa Mbezi na Kimara kutumia gharama kubwa kwenda kazini na kurudi nyumbani kwao ambapo wanatumia zaidi ya Sh 10,000.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamachinga Mkoa wa Dar es Salaam, Namoto Yusufu aliwataka vijana kutambua Tanzania ndio taifa lao pekee hakuna pengine wanaweza kuhamia endapo wataharibu nchi yao wenyewe. “Changamoto haziondolewi kwa vurugu bali kwa mazungumzo ya pamoja.Hatutaki turudishwe katika enzi za vurugu za siku ya uchaguzi. Nawasihi vijana wenzangu tusikubali kubebwa kwa mihemko na siasa za majukwaani na mtandaoni,” alisema.

Amewakumbusha vijana kuwa Rais Samia anawapenda vijana ndio maana katika Baraza lake la Mawaziri limetawaliwa na vijana na pia kwa mara ya kwanza ameunda wizara kamili inayoshughulikia masuala ya vijana.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button