SADC yazindua Mkakati wa Mawasiliano 2025/2030

JUMUIYA ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imezindua Mkakati wa Mawasiliano na Uhamasishaji ya mwaka 2025/2030 ili kuimarisha mawasiliano, uhusiano wa kikanda na maendeleo endelevu kwa nchi wanachama.
Hafla ya uzinduzi wa mkakati huo imefanyika juzi jijini Gaborone, Botswana na kushirikisha wadau wa mawasiliano, habari na washirika wa kimataifa wa maendeleo. Akizindua mkakati huo, Naibu Katibu Mtendaji wa SADC anayeshughulikia Ushirikiano wa Kikanda, Angele Ntumba amesema mkakati huo utasaidia kukuza mfumo wa mawasiliano katika karne hii ya kidijiti na kuwezesha Ukanda wa Afrika ya Kusini kuimarisha miundombinu, uchumi, biashara na miradi ya maendeleo ya jamii, kwa manufaa ya nchi wanachama.
Amesema mkakati huo wa mawasiliano uliozinduliwa katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kireno utatekelezwa kwa pamoja na nchi wanachama wa SADC chini ya waratibu wa kitaifa wa SADC na waratibu wa kitaifa wa habari na mawasiliano wa jumuiya hiyo katika nchi 16 wanachama wa SADC. SOMA: Sh milioni 403 kurejesha Mawasiliano Mbinga
Amewataka waratibu hao kushirikiana na SADC na wadau kutekeleza mkakati huo, vikiwemo vyombo vya habari na taasisi za teknolojia ya habari na mawasiliano katika nchi zao na Ukanda wa Kusini mwa Afrika. Aidha, Ntumba aliishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika lake la Maendeleo la GIZ kwa kudhamini maandalizi na uzinduzi wa mkakati huo, kwani umewezesha SADC kutekeleza majukumu yake kwa upana zaidi kupitia nyenzo muhimu ya mawasiliano na uhamasishaji.
Naye Mkuu wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ubalozi wa Ujerumani nchini Botswana, Simone Goertz alielezea azma ya GIZ kuendeleza ushirikiano na SADC kutekeleza mkakati wake wa mawasiliano na kuleta maendeleo endelevu kwa manufaa ya nchi wanachama kulingana na mabadiliko ya utandawazi yanayoendelea kutokea duniani.



