Halmashauri zitenge bajeti ya chakula mashuleni

ILI taifa lifanikiwe katika kupambana na athari za lishe duni, watoto wenye umri wa miaka sita hadi 15 wasiachwe nyuma kupata lishe shuleni. Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Mkoa wa Kagera umeonesha mafanikio makubwa katika kupunguza udumavu na utapiamlo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kutoka asilimia 44 hadi 39.

Haya ni mafanikio yanayoonesha nguvu kubwa ya serikali, halmashauri, vijiji, mitaa na wadau wa lishe. Hata hivyo, katika mafanikio hayo, kuna eneo moja la kufanyiwa kazi la lishe kwa watoto walio shuleni, hasa wenye umri wa miaka sita hadi 15.

Ukweli ni kwamba, idadi kubwa ya wanafunzi hawa hutumia saa 6 hadi 10 wakiwa shuleni bila kupata uji wala chakula cha mchana. Katika umri huu, mwili na akili za watoto zimefikia hatua muhimu ya ukuaji, wanahitaji nishati ya kutosha, vitamini na madini ili kuimarisha afya, kukua kimwili na kuweza kujifunza kwa tija.

Kukosa chakula shuleni si tu kunawafanya wawe dhaifu, bali kunachangia kuporomoka kwa uwezo wa kujifunza, kupungua kwa umakini darasani na kuongezeka kwa utoro shuleni. Kwa baadhi ya wanafunzi, uji wa asubuhi ndiyo ungeweza kuwa mlo wao wa kwanza siku nzima kabla ya chakula cha mchana au jioni, hivyo kukosekana kwa huduma hii shuleni kunawaweka katika hatari ya utapiamlo.

Jambo hilo linaweza kuathiri ubongo, uwezo wa kufikiri na mustakabali wao wa kielimu na kiuchumi baadae. Ndio maana Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza mtoto mwenye njaa hawezi kujifunza na ndicho kinachojitokeza katika baadhi ya shule za kutwa. SOMA: ‘Hakikisheni watoto wanapata chakula shuleni’

Changamoto hii inahitaji sauti ya pamoja kwa watoto walio shuleni kama inayowekwa kwa watoto wa umri sifuri hadi miaka mitano. Ni wakati wa jamii ya Kagera na kwingineko kutambua mapambano dhidi ya udumavu hayaishii tu kwa watoto wa chini ya miaka mitano, bali yanapaswa kuwa safari endelevu ya mtoto hadi amalize elimu ya sekondari.

Hivyo basi, wazazi, walezi, viongozi wa vijiji na mitaa na walimu wanapaswa kushirikiana kuweka utaratibu wa kupata uji shuleni, iwe ni michango ya hiari ya fedha, mazao au kuanzisha mashamba ya shule kama chanzo endelevu cha uhakika.

Wadau wa lishe nao waendelee kutoa elimu ya lishe bora shuleni, kusaidia vifaa vya kupikia kama majiko banifu, kuwezesha vikundi vya wanawake au wazazi kuanzisha miradi midogo ya kuchangia chakula shuleni na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa hali ya lishe kwa wanafunzi wa shule za kutwa. Pia, ni muhimu wadau kuhamasisha halmashauri kuangalia uwezekano wa kuingiza mpango wa lishe shuleni kwenye bajeti zao za maendeleo.

Hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri  ya Wilaya ya Muleba, Issaya Mbenje alitoa wito kwa wadau wa lishe wa halmashauri hiyo kuhakikisha ajenda ya chakula shuleni inakuwa ya kudumu kwa ngazi ya mikutano ya hadhara ya vitongoji na vijiji.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima kupitia mkutano wa robo mwaka wa wadau wa lishe katika wilaya hiyo alisikitishwa na wazazi wasiokuwa na moyo wa kuchangia uji kwa watoto wao shuleni na kuwaambia wadau kuwa kizazi kinaangamia na maarifa kwa watoto yanapungua, kwa sababu njaa inasababisha kupunguza usikivu.

Hatua za haraka za kunusuru kizazi hiki zinatakiwa kuchukuliwa kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni ili wasome na kucheza wakiwa na nguvu na afya. Mustakabali wa elimu, afya na maendeleo ya mkoa upo mikononi mwa kizazi hiki, tuwawezeshe kwa kuwapatia lishe bora shuleni watimize ndoto zao na za taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button