Usafiri wa mwendokasi waanza Mbagala

HUDUMA za usafi ri wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kutoka Mbagala kwenda Posta na Gerezani imerejea jana baada ya kusitishwa kwa muda. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alitangaza kusitishwa kwa usafiri huo kuanzia Novemba 5, mwaka huu kutokana na uharibifu wa miundombinu uliotokea wakati wa vurugu zilizofanyika Oktoba 29, 2025, siku ya Uchaguzi Mkuu.
Wakazi wa Mbagala wakizungumza na HabariLEO lilipotembelea kuona hali ya huduma hiyo walieleza kufarijika baada ya kurejeshwa kwa usafiri huo huku wakiwaomba wananchi kutunza miundombinu hiyo ili kuepuka adha ya usafiri. Mkazi wa Mbande, Mariam Shemdoe aliishukuru serikali kwa kurejesha usafiri huo kwa sababu awali walikuwa wakikumbana na foleni iliyowalazimu kutumia gharama kubwa kurejea nyumbani kwao.
“Tumefarijika kuona mwendokasi inarudi Mbagala. Tulikuwa tunateseka na foleni za muda mrefu sasa tunafika mjini kwa haraka zaidi, ni vizuri tukaitunza miundombinu hii, tusiharibu mabasi, vioo wala mageti, maana tumeteseka kwa muda mrefu kupata usafiri wa uhakika na wa haraka kama huu,” alisema.
Amesema hapo awali ilikuwa kawaida kusubiri muda mrefu kupata usafiri na kukaa kwenye foleni zaidi ya saa moja lakini kurejea kwa mwendokasi kumerahisisha safari, kuokoa muda na gharama. SOMA: Majaliwa akagua miundombinu BRT

Mkazi wa Mtaa wa Sabasaba Mbagala, Hamza Mpei alieleza licha ya usafiri huo kuwasaidia kuokoa muda pia kuawasaidia kuepukana na magonjwa ya kuambukiza kwa mfano homa ya ini yanayoambukizwa kwa njia ya hewa. “Kwenye mwendokasi kila mtu anakaa kwenye kiti chake hata kama umesimama utasimama kwa nafasi na kuna kiyoyozi tofauti na kwenye usafiri mwingine kwa hiyo ukipanda mwendokasi unakuwa na uhakika wa kufika haraka na salama,” alisema Mpei.
Kwa upande wake Mkazi wa Mbagala Rangi Tatu, Sikudhani Idris aliiomba serikali kuongeza mabasi hayo hasa wakati wa asubuhi na jioni ili kupunguza msongamano na watu wanaosimama. Hata hivyo HabariLEO ilizungumza na Ofisa Habari wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Elias Malima alieleza kuwa wataendelea kuboresha usafiri huo ili upatikane muda wote na kwa viwango vya kimataifa zaidi.
“Miundombinu hii inajengwa kwa fedha nyingi za umma kwa hiyo tujitahidi kuitunza kwa sababu itatusaidia sisi na vizazi vijavyo, lakini pia usafiri huu ni rafiki na salama kwa hiyo, kadiri tunavyoitunza ndivyo tunavyokuwa na uhakika wa usafiri bora,” alisema.



