Baba afanya mauaji ya mtoto kisha ajinyonga

MWANAUME mmoja, Derick Mwangama (23), mkazi wa Kijiji cha Mpandapanda, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, amemuua mtoto wake Devina Derick (2) kisha kujinyonga kwa kutumia kamba katika mti wa parachichi karibu na alipoacha mwili wa mtoto huyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema tukio hilo lilitokea Novemba 18, majira ya saa 3:00 asubuhi katika Kijiji cha Isaka, Kata ya Nkunga.
Amesema siku ya tukio, Mwangama alimchukua mtoto huyo kwa nguvu kutoka kwa mama yake, Violeth Edward (19), mkazi wa Isaka, na kutoweka naye kabla ya mwili wa mtoto kupatikana kando ya Mto Kiwira akiwa amenyongwa kwa kutumia kamba ya Manila.
Kamanda Kuzaga ameongeza kuwa mara baada ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa naye alijinyonga hadi kufa katika mti wa parachichi karibu na mwili wa mtoto wake. Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia kati ya wazazi hao ambao walikuwa wametengana.
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limetoa wito kwa wazazi na wanandoa kutatua migogoro ya kifamilia kwa njia ya mazungumzo na ushauri ili kuepusha madhara makubwa kama yaliyotokea. SOMA: Polisi Kagera yapokea kesi 279 ukatili, unyanyasaji



