Vyombo vya habari vizingatie weledi kulinda amani, uzuri wa Tanzania

MSEMAJI Mkuu wa Serikali na, Gerson Msigwa alizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kueleza jinsi baadhi ya vyombo vya habari vya nje vinavyopotosha uhalisia wa vurugu zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

Amesema katika kufuatilia, serikali imabaini nyuma ya habari hizo za upotoshaji kuna vita kuwa ya kiuchumi dhidi ya taifa hili lenye rasilimali nyingi na linalosifika kwa amani duniani. Kwa mujibu wa Msigwa, vyombo hivyo vya habari vimechapisha taarifa za upande mmoja na kuishia kusema maofisa wa serikali (ya Tanzania) walipotafutwa, hawakupatikana.

Kimsingi tunakubaliana na Msemaji Mkuu wa Serikali kuhusu uwepo wa vita vya kiuchumi inayoibuliwa kwa kigezo cha watu kudai haki ambazo pengine zingeweza kuwekwa katika meza ya mazungumzo kuliko kufanya vurugu.

Vita ya kiuchumi ina njia nyingi kutekelezwa lakini hii ya vurugu ni mbaya zaidi kwa kuwa watu wanakufa, mali zinaharibiwa na utekelezaji wa miradi unasimama huku wananchi wa kawaida nao wakishindwa kutafuta riziki ya kila siku. SOMA: BoT yatoa hakikisho usalama mifumo ya malipo

Vurugu zinapotokea kwenye taifa lolote kama ilivyotokea nchini wakati na siku chache baada ya uchaguzi kwa baadhi ya maeneo, kunaharibu biashara na kuwaongezea nguvu wapinzani wa kiuchumi. Tunaipongeza serikali kuamua kuzungumza na vyombo vya habari vya ndani kuhusu upotoshaji huu ili kwa pamoja tujifunge mkanda kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama kama ilivyo sasa.

Tunavikumbusha vyombo vya habari vya ndani kuendelea kutumia weledi na maadili ya kitaaluma kuandika habari chanya na zenye msaada kwa nchi.Tunawakumbusha wanahabari wa ndani kwamba Tanzania ni moja na ikiharibika sote hatutaweza kuishi bila kujali ni mwanasiasa, mwanataaluma, kijana, mtoto au mzee.

Mfano mmoja aliyougusia Msigwa ni maudhui ya makala iliyochapishwa na chombo cha habari cha kimataifa cha CNN kwamba chombo hicho kilivyofanya makosa ya kiudilifu na kiweledi katika uandishi wa habari kwa kuchapisha na kutangaza maudhui yanayoegemea upande mmoja.

Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, hakuishia kukosoa bali aliwaalika CNN waje upande wa serikali wasikilize na wakachapishe maudhui yenye usawa, ukweli na yasiyokuwa na mgongano wa maslahi yaliyominya sauti ya upande wowote.

Wakati serikali ikitekeleza hayo, vyombo vya ndani viendelee kufanyakazi ya kuilinda nchi kwa wivu mkubwa kwa kueleza uzuri wa Tanzania, vivutio vya utalii visivyopatikana kwingine duniani na kueleza utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayoelekea kumaliza kabisa changamoto za Watanzania, ikiwemo ajira kwa vijana.

Sasa hivi Rais Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu, hivyo sote tuiunge mkono tume hii kwa kuipa nafasi kutekeleza majukumu yake na taarifa itakayotoa, itaeleza bayana kilichotokea na kupendekeza hatua za kuchukua.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button