Madini yaweka rekodi maduhuli

WIZARA ya Madini imeingiza Sh trilioni moja katika makusanyo ya maduhuli ya sekta hiyo kati ya Julai mwaka jana na Juni 30, mwaka huu. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema makusanyo ya kiasi hicho hayajawahi kufanyika katika sekta hiyo.

Mavunde alisema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika ndani ya ukuta wa Madini ya Tanzanite Mirerani wilayani Simanjiro katika Mkoa wa Manyara jana. Amesema serikali iliipangia sekta ya madini kukusanya asilimia 10 ya makusanyo katika kipindi hicho lakini ikavuka malengo kwa kukusanya asilimia 10.1 hadi kufikia Juni 30, mwaka huu.

Mavunde amesema katika mwaka wa fedha 2015/2016, sekta ya madini ilikusanya zaidi ya Sh bilioni 161 na kwamba kiasi hicho hakikuwahi kukusanywa na sekta hiyo. Amesema kumekuwa na ongezeko la makusanyo mwaka hadi mwaka kwa kuwa wafanyabiashara katika sekta hiyo kwa sasa wanafanya biashara hiyo kwa kuzingatia sheria.

Mavunde amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza sekta ya madini kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji mapato hivyo sifa hizo ziongezwe zaidi kwa kuongeza ukusanyaji maduhuli ya sekta hiyo. SOMA: Utafiti na uendelezaji madini ya kimkakati waiva

“Tushirikiane katika ukusanyaji maduhuli ya serikali na tuwafichue watorosha madini kwani baadhi yao bado wanafanya biashara hiyo kupitia mpaka wa Rombo,” alisema. Katibu wa Wafanyabiashara Wakubwa wa Madini Nchini (TAMIDA), Leopod Kimaro alimuomba waziri kuwakutanisha na wizara ya fedha ili kutatua changamoto za kikodi.

Waziri amekubali ombi hili akisema muda wowote watakutana ili pande zote ziweze kufanya biashara kwa amani na kila mmoja afaidike na biashara hiyo. Aidha, Mavunde amegawa leseni zaidi ya 20 kwa wachimbaji wadogo wa uchimbaji madini ya Tanzanite. Tanzania iwe Dubai ya madini Mavunde alisema anataka Tanzania kiwe kituo cha biashara ya madini kama Dubai.

Amesema anatamani Tanzania itumie mfumo wa madini unaotumika Dubai na atalivalia njuga jambo hilo. Mavunde alisema serikali ipo katika mkakati wa kuongezea thamani ya madini ya Tanzanite katika soko la dunia. Amesema Rais Samia ameagiza sekta ya madini iongeze mchango wake katika uchumi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wafanyabiashara wakubwa, kati na wachimbaji wadogo wanafanya biashara ya madini hayo kwa njia sahihi yenye kuongezea pato taifa.

Mavunde amesema njia ya kuliongezea thamani jiwe la tanzanaiti ni pamoja na kurejesha maonesho ya kimataifa ya madini ya vito, minada ya kimataifa kufanyika katika mji wa Mirerani. “Serikali imejipanga kuhakikisha inarudisha ukuu wa Tanzanite na madini hayo yanakuwa na thamani kubwa muda wote katika soko la kimataifa. Tunaomba ushirikiano kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa, kati na wadogo katika kuipa thamani Tanzanite ili serikali ifikie malengo yake,”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button