Dk Akwilapo ataka utu sekta ya ardhi

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo ameagiza watumishi wa sekta ya ardhi wazingatie utu wakati wa kuhudumia wananchi. Aidha, amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa umakini, uadilifu na wazingatie miongozo ya utumishi wa umma wakati wote wa kutekeleza majukumu yao.
Dk Akwilapo ametoa maagizo hayo alipotembelea kliniki ya ardhi inayoendeshwa katika Mtaa wa Mbae Mashariki na Likombe katika Halmashuari ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara jana. “Falsafa ya Rais ni kuwaacha wananchi kuwa na furaha kwa kuondoa migogoro ya ardhi,” alisema.
Dk Akwilapo amewataka wananchi wa Mtwara wahakikishe wanamilikishwa maeneo yao kwa kupata hati milki za ardhi na kuwa na vibali vya ujenzi wanapotaka kuendeleza maeneo yao ili kuepuka migogoro. SOMA: Hati za ardhi zatolewa kwa wakazi wa Sikonge
Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Mtwara, Fredrick Mrema amesema katika kliniki ya ardhi inayoendelea katika Halmashauri ya Mtwara Mikindani, takribani hati milki za ardhi 503 zimetolewa kwa wananchi wa mitaa ya Mbae na Likombe. “Zoezi hili la kliniki ya ardhi ni endelevu na lengo letu tumepanga kuhudumia wananchi 10,984 katika kata nne za halmashauri hii ya Mtwara Mikindani,” alisema Mrema.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya amewahimiza wananchi wilayani humo kuhakikisha wanamiliki maeneo yao kwa kupatiwa hati milki za ardhi. “Wananchi nawaombeni mmiliki maeneo yenu kwa kuwa na hati milki, hati ya ardhi inakupa uhakika wa milki na kilichofanywa na wizara katika kliniki hii ya ardhi kuwapatia wananchi hati ni jambo kubwa na la kihistoria,” alisema Mwaipaya.



