Washitakiwa 1,736 vurugu za uchaguzi kuachiwa

SERIKALI imetangaza washitakiwa 1,736 kati ya 2,045 waliokamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya kula njama na uhaini kutokana na vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu, wataachiwa. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera ametangaza hayo katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Njedengwa mkoani Dodoma.
Dk Homera amesema Novemba 18, mwaka huu Rais Samia alitoa msamaha kwa walioshiriki maandamano kwa kujua au kutokujua na kwa mujibu wa takwimu alizozitoa ni kuwa kulikuwa na jumla ya waandamanaji 2,045 walikamatwa nchi nzima kutokana na tukio hilo. SOMA: Niffer akwama, wenzake 20 wafutiwa mashitaka
Amesema kutokana na maelezo ya Rais Samia watakaoachiwa kwa sasa ni 1,736 na hadi Novemba 25, mwaka huu walikuwa wameachiwa 607 na bado wanaendelea kuwaachia baada ya upekuzi wa kina na kujiridhisha ili waweze kutoka. “Na zoezi linaendelea lakini katika hao 2,045 watu 309 kazi ya ufuatiliaji bado inaendelea lakini kwa kweli watakaoachiwa ni 1,736 kati ya hao na walioachiwa hadi tarehe 25 ni watu 607,” alisemaa Dk Homera.
Akitaja takwimu za walioachiwa kwa mikoa alisema Manyara aliachiwa mmoja, Mwanza 164, Arusha 24, Geita 74, Dar es Salaam 263, Rukwa 10, Mbeya 69 na Shinyanga watu wawili na bado wanaendelea kuachiwa.



