Samia: Tumejipanga, tutailinda Tanzania

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali yake itailinda Tanzania kwa nguvu zote.

Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rais Samia amesema waliohamasisha vurugu siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu na siku zilizofuata walipanga kuangusha dola lakini serikali imeapa kuilinda nchi.

“Tunaapa kuilinda nchi hii na mipaka yake, kulinda usalama wa raia na mali zao, na katika hali hiyo nguvu inayotumika inaendana na tukio lililopo. Tunapoambiwa kwamba tulitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo ilikuwa ni ipi,” Rais Samia alihoji mbele ya wazee hao na viongozi wa serikali.

Aliongeza: “Kuna mengine nasikia yanapangwa lakini Inshallah Mola hatosimama nao… litapeperuka.“Lakini nataka niseme nilimsikia mmoja kati ya waandaaji wa nje anasema tarehe 9 (siku waliyopanga maandamano) iahirishwe isubiriwe siku ya Krisimasi, sababu sasa hivi tumejipanga… nataka niwaambie, wakati wowote wakija tumejipanga.”

Rais Samia aliongeza kuwa waliapa kuilinda nchi, raia na mali zao kama wanavyofanya mataifa mengine na Watanzania hawawaingilii, vivyo hivyo na Tanzania inafanya kwani ni nchi huru ya kidemokrasia.

SOMA: Rais Samia aunda Tume Huru kuchunguza vurugu za uchaguzi

“Niseme tu kwa ufupi kwamba vurugu za tarehe 29 na 30 si desturi wala utamaduni wa Watanzania. Kila aliyeumia au kupoteza maisha ni Mtanzania mwenzetu mwenye haki sawa na wengine… hakuna aliye juu ya mwingine.

“Haki ya kuishi na kuwa huru ni tunu zetu wote Watanzania, kwa hiyo hakuna sababu ya Watanzania kuumizana na kunyimana uhuru. Inatia uchungu kuona wachache walioratibu fujo zile wakitaka Watanzania wenzao wawe kafara kwa malengo yao ya kisiasa yaliyojaa ubinafsi, tofauti na siasa iliyopo,” alisema Rais Samia.

Alisema lililotokea ni tukio la kutengenezwa na waliolitengeneza walidhamiria kuangusha dola na walihamasishwa kufanya yaliyotokea Madagascar bila kujua wanachotaka.

“Vijana wetu waliimbishwa kama kasuku… ukimuuliza Madagascar kilitokea nini hajui, unataka hapa kitokee nini hajui lakini waliimbishwa wimbo huo. Kwa hiyo, lile lilikuwa ni jambo la kupangwa na vurugu zile zilidhamiria makubwa… vurugu zile ni mradi mpana sana,” alibainisha kiongozi huyo wa nchi.

Alisema kwa sababu zozote, Watanzania hawakupaswa kuvuruga amani ya nchi wala kusababisha vifo kwa watu.

“Kwa hiyo, kwa wale waliondokewa na ndugu zao na jamaa zao na watoto zao, natoa tena pole kwa sote, si msiba wao peke yao, ni wetu wote kwani damu ya Watanzania ni yetu sote. Mtanzania mmoja akiumia, tumeumia  wote kwa hiyo tuwe pole wote,” alieleza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alihoji mataifa yanayodai serikali ilitumia nguvu kubwa kudhibiti vurugu, akisema walitaka kifanyike kitu gani ilihali vijana walikuwa wanachoma nchi.

“Tunaapa kuilinda nchi hii na mipaka yake, kulinda usalama wa raia na mali zao na katika hali hiyo, nguvu inayotumika inaendana na tukio lililopo. Sasa tunapoambiwa kwamba tulitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio hilo, nguvu ndogo ilikuwa ipi? Ilikuwa tuwangalie waandamanaji waliojiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe, hapo kutakuwa na dola?” alihoji.

Aliwataka wazee kuzungumza na vijana kuwaelekeza namna ya kuishi na kuipenda nchi yao na kukiri mambo hayo yanatokea kwa vile vijana hawajafundishwa uzalendo.

“Haya yote yanatokea, tumejifunza sababu vijana wetu tumewaacha wakakua wenyewe, wanajiongoza wenyewe kwa hiyo hawana mwelekeo, hawana watu wa kuwaongoza vizuri, kwa hiyo hawana elimu ya uzalendo.

“Vijana wazalendo hata kutoka vyama vya upinzani hawakukubaliana na hali ile, wakatuambia kuna hili linapangwa kaeni vizuri. Tumejifunza, tutakwenda kulifanyia kazi na ndio maana nikasema niunde wizara nzima ya vijana ili kushughulika na vijana kwa upeo mpana,” alifafanua Rais Samia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button