Kimiti ahimiza haki, amani

KIONGOZI mstaafu wa serikali, Paul Kimiti amesema kuwe na haki, kwa kuwa si rahisi kutenganisha haki na amani.

Kimiti alieleza hayo wakati wa mazungumzo yake katika kipindi cha dakika 45 kilichorushwa na kituo cha
Televisheni cha ITV.

Kimiti alisema haki ni vile vitu vya msingi ambavyo binadamu anapaswa kuvipata na viongozi wakitenda haki na amani itakuwepo lakini wasipotenda haki, amani haitakuwepo.

“Hayo ni mambo si rahisi kuyagawa ukitenda haki, amani itakuwepo lakini usipotenda haki, amani hutaipata. “Hiyo kazi ni kubwa si ndogo, lazima tuifanye. Tunaandaa namna gani vijana wetu ili waone haki si haki tu hovyo hovyo kujikalia kupata haki,” alisema.

Alisema amani ni msingi ambao watu wote wanahitaji na kuishi kama familia.

Akizungumzia suala la uzalendo kwa nchi, Kimiti alisema uzalendo ni kuipenda, kuitumikia na kuiheshimu nchi na taratibu zake, akisisitiza ni muhimu vijana wakapatiwa mafundisho na elimu.

Sambamba na hilo, Kimiti alieleza namna madhehebu ya dini yanapaswa kuepuka kubaguana na kuchafuana, akisisitiza kutumia njia ya mazungumzo kama kuna changamoto ili kuzitatua kwa njia sahihi na sio ya kuwagawa watu kwa kigezo cha dini.

“Tusianze sasa kubaguana kwa madhehebu, itatufikisha pabaya sana… hata kama kuna lolote, hapa kuna tume ya amani ambayo madhehebu yote yanakutana kama kuna lolote. Kwa nini msizungumze mkayamaliza kimyakimya?” alihoji.

Aliendelea: “Tusiache amani ikapotea, tutakuja kugharamia gharama kubwa sana kuirudisha amani. Lazima tuanze kuzuia pale inapotokea (misuguano).”

Akizungumzia suala la vijana, alisema serikali imefanya jambo sahihi kuanzisha Wizara ya Vijana kwa ajili ya kutambua matatizo ya vijana na kutafuta suluhu na kufahamu matakwa yao.

Aliitaka wizara hiyo kuja na mipango madhubuti ya kuhakikisha vijana hawasahauliki na wanashirikishwa katika masuala yanayowahusu.

Pia, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa falsafa yake ya ‘Kazi Iendelee’ iliyowezesha kuendeleza yale yalioyoachwa na watangulizi wake.

Alisema kwa sasa nchi imepiga hatua kwa kiasi kikubwa katika kufanya maendeleo ya sekta zote.

“Niliwahi kusema amefanya kazi kuliko hata wanaume. Nilisema utendaji wa kazi amefanya kazi vizuri, tuna imani kabisa na tunataka tumsaidie aishi katika amani utulivu na umoja,” alisema.

Kadhalika, Kimiti alihimiza suala la maadili mema kwa viongozi wa serikali kuwatumikia wananchi na kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhilifu, akiwataka waenzi misingi ya viongozi wa zamani waiyoidumisha.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button