Tume ya Uchunguzi ina ‘kibarua kizito’ lakini muhimu

KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 74 inaelekeza kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kila baada ya miaka mitano.
Ni kwa msingi huo, Oktoba 29, 2025 nchini Tanzania ulifanyika uchaguzi huo ukiwa ni wa saba katika mfumo wa siasa wa vyama vingi uliorejea nchini mwaka 1992.
Uchaguzi Mkuu wa Kwanza ulifanyika mwaka 1995 na uchaguzi wa sita ulifanyika mwaka 2020 ukifuatiwa na wa mwaka huu uliomweka madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan.
Licha ya kukamilika kwake, Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu umeshuhudia siku ya kupiga kura na siku tatu baadaye kukiwa na ghasia zilizoambatana na vitendo vya uvunjifu wa amani katika baadhi ya maeneo ya miji ya mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Geita, Mara, Mbeya, Mwanza na Songwe.
Vitendo hivyo vilisababisha vifo, majeruhi, uporaji, uharibifu wa miundombinu na mali za umma pamoja na mali za watu binafsi.
Hali hiyo, ndiyo iliyosababisha Rais Samia kwa mujibu wa Kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, Toleo la Mwaka 2023, Novemba 20, 2025 kuunda na kuzindua Tume Huru ya Kuchunguza Matukio ya Ghasia na Uvunjifu wa Amani Yaliyotokea Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Kimsingi, tume hiyo ina kibarua kizito lakini muhimu kwa mustakabali wa taifa hivyo, inastahili ushirikiano wa kila Mtanzania kwa manufaa ya Watanzania na taifa lao. Tume inaundwa na wajumbe tisa ikiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Mohamed Othman Chande.
Wajumbe wake ni Jaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ambaye ni mwanadiplomasia; Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue na mwanadiplomasia na Balozi Mstaafu, Radhia Msuya.
Wajumbe wengine ni wanadiplomasia na mabalozi wastaafu Luteni Jenerali Paul Meela, George Madafa, David Kapya, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IJP) mstaafu, Said Mwema na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk Stergomena Tax.
Katika mazungumzo na waandishi na wahariri wa vyombo vya habari Dar es Salaam juzi, Jaji Chande anasema, “Uteuzi wa wajumbe hawa unazingatia Sheria ya Uchunguzi, Sura ya 32 inayompa rais madaraka ya kuagiza uchunguzi katika jambo lolote ambalo anaona lina manufaa kwa umma.”
Kwa nini Tume
Jaji Chande anasema, “Lengo la kuundwa kwa tume hiyo ni kuchunguza kwa kina kiini cha ghasia zilizojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu… lengo hilo linaakisi hadidu za rejea zilizotolewa kwa tume ambazo zinajikita katika nguzo tano za kiuchunguzi ambazo ni chanzo cha ghasia, wahusika, madhara na hatua zilizochukuliwa na serikali kuzuia na kudhibiti matukio ya uvunjifu wa amani.”
Anaongeza: Tume itapendekeza maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi ili kuongeza uwajibikaji wa viongozi na raia katika kulinda amani, utawala wa sheria, haki za binadamu, utawala bora na mfumo thabiti wa majadiliano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii hadi kufikia maridhiano ya kitaifa na kuhakikisha vurugu kama hizo hazitokei tena.”
Ndio maana wadau wa amani na maendeleo ya taifa wanasema, tume ina kibarua kizito lakini muhimu kwa mustakabali wa taifa na inastahili ushirikiano wa kila Mtanzania.
Anabainisha kuwa, katika kutekeleza majukumu, tume hiyo inaongozwa na hadidu za rejea sita ambazo ni kuchunguza na kubainisha chanzo cha halisi cha ghasiahizo, kuchunguza na kubaini lengo kuu lililokusudiwa na waliohusika kupanga na kutekeleza vitendo hivyo vya ghasia na uvunjifu wa amani pamoja na kuchunguza na kubainisha madhara yaliyotokea kutokana na ghasia hizo, ikiwamo vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na miundombinu pamoja na madhara ya kiuchumi na kijamii.
Nyingine ni kuchunguza mazingira na hatua zilizochukuliwa kubaini na kukabiliana na ghasia zilizojitokeza na kuchunguza jambo lolote ambalo tume itaona ni muhimu na linaendana na majukumu yake.
Hadidu nyingine Jaji Chande anasema ni: “Kupendekeza maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi ili kuongeza uwajibikaji wa viongozi na raia kulinda amani, utawala wa sheria, haki za binadamu, utawala bora na mfumo thabiti wa majadiliano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii hadi kufikia maridhiano ya kitaifa na kuhakikisha vurugu kama hizo hazitokei tena.”
Kwa mujibu wa Jaji Chande, uchunguzi utahusisha maeneo yaliyoathirika zaidi na ghasia kwa upande wa Tanzania Bara ili kubaini aina za matukio, chanzo, athari na hatua zilizochokuliwa kuzuia na kudhibiti hali hiyo. “Vilevile, itatembelea baadhi ya maeneo ambayo hayakuwa na ghasia ili kujifunza mazingira yaliyochangia hali hiyo,” anasema.
Anasema Sheria ya Tume ya Uchunguzi inaipa mamlaka tume kumwita au kumwalika mtu yeyote kwa ajili ya mahojiano kupata taarifa zitakazosaidia katika uchunguzi. “Tunatoa wito kwa Watanzania wote kutoa ushirikiano ili tume iweze kupata taarifa sahihi na kwa wakati.”
Anaongeza: “Tume pia imepanga kufanya baadhi ya mahojiano yake na wadau mbalimbali na wataalamu kwa njia ya wazi.” “Mikutano mingine itafanyika katika hadhara na mingine kwenye faragha katika mazingira maalumu ili kulinda haki ya faragha… tutafanya uchunguzi uliokamilika kwa uwazi na kwa kuzingatia usalama wa watoa taarifa. Tutafanya uchunguzi wa kina na wa kitaalamu, hata kwa kutumia data na kwa kweli tume haitaacha jambo lolote bila kujulikana.”
Akizungumzia methodolijia, Jaji Chande anasema tume itatumia njia mbalimbali kuiwezesha kupata taarifa sahihi na za kina, zikujumuisha mapitio na uchambuzi wa nyaraka pamoja na mahojiano ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao.
Nyingine ni dodoso la mtandaoni, baruapepe, barua za kawaida, ujumbe mfupi wa simu, kutembelea uwandani, mijadala na makundi mbalimbali na ushauri wa kitaalamu. “Tunaamini kwa kutumia njia zote hizo, tutapata taarifa zote muhimu na tutawafikia wadau wengi,” anasema.
Kwa mujibu wa tume, wadau watakaoshirikishwa watatoka katika makundi mbalimbali ya jamii, wakiwamo waathirika, watuhumiwa, vyama vya siasa na asasi za kiraia.
“Moja ya kazi za tume ni kuanza kuponya…” anasemana kufafanua: “Hatuna mamlaka ya kijinai; hatushitaki mtu…” Wengine ni wasimamizi wa uchaguzi na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), viongozi wa dini, viongozi wa bodaboda, viongozi wa wamachinga, wafanyabiashara na wajasiriamali.
Anasema wengine watakaoshirikishwa ni wadau wa maendeleo, watu mashuhuri, mamlaka za serikali za mitaa hasa katika maeneo yaliyoathirika zaidi, wakuu wa taasisi za serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, sekta binafsi za ulinzi, waandishi wa habari, watafiti pamoja na wataalamu wa sekta na fani mbalimbali.
Anasema uchambuzi wao wa haraka umebaini matarajio kadhaa ya Watanzania katika tume hiyo ni pamoja na “Uchunguzi uliokamilika na kwamba usifanyike nusunusu; tuwe wawazi kufanya kazi na wanatarajia tuchukue ushahidi utakaotumika, si ambao hauwezi kutumika.”
Kadiri ya maelekezo ya Rais Samia, tume inatarajia kukamilisha kazi yake ndani ya siku 90 tangu ilipoanzishwa na kukabidhi taarifa kwa rais. Anasema, “Kuanzia sasa, tume ipo tayari kupokea taarifa na maoni kupitia tovuti ya tume kwa anuani ya https://www. tume.uchunguzi.go.tz; baruapepe: maoni@tume.uchunguzi.go.tz, simu na ujumbe mfupi wa simu kupitia namba 0743040890 na 0737305449.”
Anasisitiza, “Tume hii ni huru kabisa kwa mujibu wa sheria na inaelewa vyema majukumu yake na inatambua uzito wake. “Ahadi yetu ni kutekeleza majukumu hayo kwa weledi, uadilifu na uwazi ili kuleta majibu sahihi. Natoa rai kwa vyombo vya habari na wananchi wote kutoa ushirikiano kwa tume kwa maslahi mapana ya taifa letu.”
Anaongeza: “…Pamoja na uchungu mkubwa tuliopata, majibu ya mambo mengi tunayo sisi wenyewe na majibu ya msingi ndiyo yatatusaidia tufanye nini.”
Katika majadiliano na kujibu maswali ya wahariri, Jaji Chande anasema: “Tunajua msimamo wa vyama vingine; tume tutaomba ushirikiano wao, maana si ajabu baadhi ya watu kutoshirikiana na tume za namna hii. “… Tutawaomba tushirikiane, maana pia tumeombwa tupendekeze hatua za kuifanya Tanzania kuwa salama na yenye amani, likiwamo suala la katiba mpya… Kila mtu hata aliyekataa tutamwomba na kumbebeleza ashirikiane na tume…”
Hata hivyo, anasema katika kuangalia kiini hasa cha vurugu, tume itaangalia hata mambo mbalimbali ya nyuma kabla ya siku ya uchaguzi ili kupata kiini hasa cha tatizo.
Anasema, “Tutajikita kwenya hadidu za rejea tukianzia sifuri, kwani hatuna amri ya mtu yeyote na tumeanza kazi bila shinikizo la mtu yeyote. Tutakuwa na mbinu mbalimbali shirikishi kwa vijana, wasomi na wasiosoma; wenye ajira na wasio na ajira, maana hatutawahoji kama tuhuma, bali kupata majawabu.”
Anaongeza: “Tutafanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na kwa viwango tukijua tunapimwa na Watanzania ndani na nje ya Tanzania. Hivyo, tusipimwe kabla ya mtihani (kazi), bali tupimwe baada ya mtihani.”
Kimsingi, tume ina kibarua kizito lakini muhimu kwa amani ya taifa ambayo ni mtaji na rasilimali ya thamani kuliko kitu kingine chochote. Ndio maana wadau wengi wanasema, “Amani Yetu, Maisha Yetu, Maendeleo Yetu, Tuijenge, Tuitunze na Tuilinde.”



