BOT, NBAA kuimarisha mifumo ya kidijitali

DAR ES SALAAM: Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) zimesaini makubaliano mapya ya ushirikiano (MoU) yenye lengo la kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali, kuongeza uadilifu katika uandaaji wa taarifa za kifedha, na kuboresha mazingira ya usimamizi wa fedha nchini.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa 25 wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu unaoratibiwa na NBAA, mkutano unaowakutanisha washiriki zaidi ya 4,500 kutoka sekta binafsi na ya umma, wakiwemo wajumbe kutoka nje ya nchi.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba, amesema hatua hiyo itaongeza nguvu katika kuziwezesha taasisi na wataalamu wa uhasibu kutumia mifumo ya kisasa inayoongeza uhalisia wa taarifa za kifedha na kudhibiti mianya ya udanganyifu.

“Sisi kama Benki Kuu tumepata fursa kusaini makubaliano haya ambayo yanalenga kuongeza ushirikiano baina ya BOT na NBAA, hususan katika kuwezesha wakaguzi na wahasibu kufanya kazi kwa kutumia mifumo ya kidijitali ili kuongeza uadilifu na usimamizi bora wa masuala ya kifedha kwa maslahi mapana ya taifa,” amesema Tutuba.
Ameongeza kuwa BOT itaendelea kuhakikisha mifumo ya malipo nchini inakuwa salama, ikiwemo kuimarisha usimamizi wa usalama mtandao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, Profesa. (CPA) Sylvia Temu, amesema makubaliano hayo yataongeza uwazi na kuaminika kwa taarifa za kifedha zinazotolewa na wakaguzi na wahasibu waliorejistishwa na bodi hiyo.
“Mkataba huu utatusaidia kuhakikisha taarifa zote za ukaguzi zinazowasilishwa NBAA kimtandao zinakuwa na credibility ya juu, zinatumika na wadau kama benki, TRA na wawekezaji bila kubabaisha. Hii itaongeza thamani na uaminifu katika tasnia yetu,” amesema Prof. Temu.
Amebainisha pia kuwa maendeleo ya teknolojia na viwango vipya vya uandaaji wa hesabu vinavyolenga uendelevu (sustainability reporting) vitahitaji wahasibu kuwa na ujuzi wa ziada na kuendelea kuzingatia maadili, ili kuendana na matarajio ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania katika miaka 25 ijayo.
Mshiriki wa mkutano huo, ACPA Magdalena Osima, ambaye ni Meneja Mkuu wa Halisi Microfinance Limited, amesema ameona makubaliano kati ya BOT na NBAA kama hatua muhimu itakayowezesha taasisi mbalimbali kupata taarifa za kifedha kwa urahisi zaidi kupitia teknolojia. Amesema matumizi ya mifumo ya kisasa yataongeza ufanisi na kusaidia taasisi kunufaika na taarifa sahihi, hivyo kuongeza uwezo wa kufanya maamuzi bora katika sekta ya fedha.
Mkataba huo unatarajiwa kuimarisha uandaaji wa taarifa za kifedha kwa kutumia mifumo ya kidijitali, kurahisisha upatikanaji wa data, na kuongeza ushirikiano kati ya wadau wakuu wa uchumi.




Epuka kujiunga au kushiriki kwenye makundi ya mtandaoni yanayochochea vurugu. Ni kosa kwa mujibu wa sharia.