Mapingamizi yasimamisha uchaguzi wa mwenyekiti Chato

GEITA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita kimesimamisha kwa muda mchakato wa uchaguzi wa mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kufuatia mapingamizi ya mgombea mmoja.

Uamuzi huo wa CCM Mkoa wa Geita umepelekea kukwamisha zoezi la uapisho wa madiwani wateule wa kata zote halmashauri ya wilaya ya Chato ambao wote ni wanachama wa CCM.

Mapingamizi yanadaiwa kuwasilishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo aliyemaliza muda wake, Christian Manunga (CCM) ambaye alishindwa katika mchakato wa uchaguzi wa ndani wa chama.

Katibu wa CCM wilaya ya Chato, Charles Mazuri ametoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa Habari ofisi kwake na kueleza uamuzi huo ulipekea Baraza la Madiwani la kwanza kutoendelea.

Amesema matokeo ya uchaguzi wa ndani yalimpitisha Diwani mteule wa Kata ya Muungano, Charles Kapembe kuwa mgombea pekee wa nafasi ya uenyekiti kwa kupata kura 20 kati ya 34.

Amesema mchakato wa uchaguzi wa ndani ulifanyika Desemba 01, 2025, baada ya kupokea wagombea waliopitishwa na halmashauri kuu ya CCM taifa na uchaguzi ulikuwa huru na haki.

Amesema baada ya uchaguzi wa ndani wagombea wote walisaini hati ya uchaguzi kuonyesha kuridhishwa na mwenendo wa uchaguzi na kukiri uhalali wa idadi ya kura zilizopigwa.

“Kwa hiyo tulihesabu kura na mshindi akapatikana, Manunga akapata kura 14, na Kapembe akapata kura 20, tulitangaza tukamaliza” amesema na kuongeza;

“Tulimaliza, tukatangaza, na kura zikahesabiwa ukumbini hapohapo, na kila mgombea alielekezwa kuchukua kura zake kupitia kwa mawakala wao.”, ameeleza Mazuri.

Amesema maelekezo ya kusitishwa kwa mchakato wa uchaguzi na uapisho wa madiwani yalisomwa na mkurugenzi wa halmashauri na kueleza barua hiyo imetoka CCM mkoa wa Geita

Mgombea Uenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Chato, Diwani Mteule kata ya Muungano, Charles Kapembe amesema ameshitushwa na hatua hiyo kwani ni kama ameporwa ushindi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM kata ya Muungano, Edward Lubinza amesema uamuzi huo unatia doa demokrasia ndani ya chama inayosimamiwa na Mwenyekiti wake Dk Samia Suluhu.

Mwenyekiti wa CCM kata ya Kasenga, Josephat Mketani ameomba uongozi wa CCM taifa kufuatilia uamuzi huo kwani wagombea waliopigiwa kura ni waliopitishwa na halmashauri kuu.

Diwani Mteule wa Kata ya Chato (CCM), Mange Ludomya amekiri kushuhudia mchakato wa wazi wa uchaguzi ndani ya CCM na hawakutegemea pingamizi hilo ambalo lililokwamisha kiapo chao.

Habari Zifananazo

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button