MCF kuleta mageuzi sekta ya afya

DAR ES SALAAM: ILI kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa nchini na kupatikana kwa wingi, Taasisi ya Medical Credit Fund (MCF), imetambulisha rasmi mfumo wa Afya Mkopo wenye lengo la kuleta mageuzi katika sekta ya afya nchini na kuisaidia serikali na kuhakikisha huduma za afya zinamfikia kila mwananchi hadi kufikia mwaka 2030.

Akizungumza leo, Desemba 4, 2025, katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuwahusisha viongozi wa MCF pamoja na wadau mbalimbali wa afya, Mkurugenzi Mkazi wa MCF, Dk. Heri Marwa, amesema kuwa mfumo wa Afya Mkopo utawezesha kupungua kwa vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano na vifo vya akina mama wajawazito.

Dk. Marwa amebainisha kuwa, kupitia ushirikiano kati ya MCF na Vodacom, tayari watu zaidi ya 100 kutoka mikoa mbalimbali wamenufaika na mikopo hiyo. Walionufaika ni wamiliki wa maduka ya dawa muhimu, hospitali na kliniki, ambao wametumia mikopo hiyo kuongeza mitaji, kununua vifaa tiba na kuhakikisha upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa.

Kwa upande wake, Mshauri wa Biashara Delfina Thomas amesema kuwa kiwango cha chini cha mkopo kinachotolewa ni shilingi 200,000, huku kiwango cha juu kikiwa shilingi 100,000,000, ambapo ameongeza kuwa mikopo hiyo inapatikana kwa urahisi, na imelenga kusaidia wamiliki wa maduka ya dawa, hospitali na maabara kupata fedha za haraka ili kukuza biashara zao.

Naye Meneja wa Mipango na Ripoti wa Vodacom M-Pesa, Hellen Komba, amesema kuwa huduma ya Afya Mkopo inakwenda sambamba na dira yao ya kuwafikia wananchi kupitia huduma za kifedha, na kwamba kwa kupitia ushirikiano huo, wafanyabiashara wa sekta ya afya watanufaika zaidi na mikopo yenye masharti nafuu.

Mmoja wa wanufaika wa mkopo huo, Thadei Mlacha, Meneja wa Biashara kutoka Nakiete Pharmacy, ameishukuru MCF kwa kuanzisha mfumo wa Afya Mkopo, kwasababu huduma hiyo itawasaidia wafanyabiashara kukabiliana na changamoto za kifedha zinazohusiana na ununuzi wa vifaa tiba na dawa.

“Sisi kama wafanyabiashara tumeipokea katika mtazamo chanya kwasababu zipo nyakati ambazo kama mfanyabiashara unapitia changamoto za kifedha kwaajili ya kuweza kufanya manunuzi kwaajili ya kupata dawa na kuhakikisha kwamba wagonjwa ama wateja wanapata dawa wakati wote. Pia nitoe rai kwa wafanyabiashara wenzangu ambao hawakupata mwaliko huu kwamba wakimbiie Afya Mkopo kwasababu ni huduma ambayo ina masharti nafuu hasa kwa mtu ambaye imejisajili na huduma ya Lipa kwa M-Pesa na mkopo wao unariba ndogo zaidi” amesema Mlacha.

Habari Zifananazo

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button