937,581 kujiunga kidato cha kwanza

OFISI ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imesema wanafunzi 937,581 wamechaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwakani. Waziri wa Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe amesema wanafunzi hao ni sawa na asilimia 100 ya wanafunzi waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar r-es-salaam , Profesa Shemdoe kuwa uchaguzi wa wanafunzi hao umezingatia kigezo cha ufaulu wa mtahiniwa anayepata alama za ufaulu kati ya 121 hadi 300. SOMA: Mtihani wa darasa la saba kuanza kesho
“Uchaguzi huu umehusisha wanafunzi 937,581 sawa na asilimia 100 ya wanafunzi wote waliokuwa na sifa ya kuchaguliwa; kati ya hao wasichana ni 508,477 na wavulana 429,104. Wanafunzi hao ni wale waliofanya na kufaulu mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2025,” alisema.
Profesa Shemdoe amesema wanafunzi wenye mahitaji maalumu 3,228, wakiwemo wasichana 1,544 na wavulana 1,684 wamepangwa katika shule za sekondari za serikali 5,230 kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza.
“Wanafunzi waliochaguliwa shule za wenye ufaulu wa alama za juu ni wanafunzi 815, huku wasichana wakiwa 335 na wavulana 480,” alisema. Ameongeza: “Tayari wamepangiwa shule za sekondari ambazo hupokea wanafunzi wenye ufaulu wa alama za juu. Shule hizo ni Ilboru, Msalato, Kibaha, Kilakala, Mzumbe, Tabora Boys na Tabora Girls.”
Profesa Shemdoe amesema wanafunzi waliochaguliwa shule za amali za bweni ni 3,441, wakiwemo wasichana 1,279 na wavulana 2,162. Alisema wanafunzi waliochaguliwa shule za bweni za kitaifa ni 7,360, wakiwemo wasichana 5,014 na wavulana 2,346.
“Katika mgawanyo huo, wanafunzi 925,965 wakiwemo wasichana 501,849 na wavulana 424,116 wamechaguliwa kujiunga katika shule za sekondari za kutwa ambazo hupokea wanafunzi kutoka katika eneo la karibu na shule ya msingi aliyosoma mwanafunzi husika,” alisema Profesa Shemdoe.
Amesema serikali imekwishafanya maandalizi ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu wanajiunga na elimu ya sekondari ifikapo Januari 2026. Aidha, Profesa Shemdoe aliwaasa wanafunzi waliochaguliwa watumie fursa waliyoipata kwa kusoma kwa bidii ili wafikie malengo waliojiwekea na matarajio ya wazazi.
Profesa Shemdoe aliiagiza mikoa na halmashauri zote wahakikishe wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka wa masomo 2026 wanaripoti shuleni na kuandikishwa ili kupata haki yao ya msingi ya elimu.



