Karume, Shein wataka elimu ya Muungano idumishwe

RAIS Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi awamu ya sita Dk Amani Abeid Karume pamoja na Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Awamu ya Saba Dk Ali Mohamed Shein wameitaka Ofisi ya Makamu wa Rais kuendelea kutoa elimu ya kutosha ya Muungano ili misingi ya Muungano iliyowekwa na waasisi iendelee kudumishwa.

Marais wastaafu hao, wameyasema hayo kwa nyakati mbili tofauti wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni alipowatembelea viongozi hao huku akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Ofisi ya Makamu wa Rais.

Dk Karume amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuuendeleza umoja huu hususani katika ulimwengu wa sasa, hii itasaidia kuwa na umoja zaidi na hili ndio litatufanya kuwa imara kwa kuangalia mifano ya mataifa mengine.

SOMA: Msekwa afichua siri ya kuzaliwa Muungano

Amesema wengi wanauonea wivu Muungano wetu hivyo kitakachotusaidia ni kuendelea kuimarisha umoja, mshikamano na kuendelea kuwaelimisha vijana wetu ili wafahamu sababu na umuhimu wa kuwepo kwa Muungano.

“Sisi tuliokuwepo tulibahatika kuwauliza wazee wetu sababu ya wao kuuweka Muungano huu, lakini vijana hawa wanapaswa nao wafahamishwe faida na misingi ya Muungano maana hawajui hivyo wanatakiwa kuelimishwa, hata sisi tulipofanikiwa kuingia kwenye uongozi tulihakikisha tunauimarisha umoja huo,” amesema.

Kwa upande wake Dk Shein amesema watu wamekuwa wakisahau na hawakumbushani nini kilichokuwa chanzo cha Muungano, hivyo ni vyema Ofisi ya Makamu wa Rais ikafanya jitihada ya kusaidia wengine kujua faida ya umoja huu na hii itasaidia kuudumisha Muungano.

“Elimu ikitolewa vizuri itasaidia vijana ambao bado hawana uelewa wa kutosha wa Muungano wetu, kuelewa. Watu wengi ambao wamezaliwa baada ta Mwaka 1964 hawaufahamu Muungano na hiyo imepelekea wao kutoa kauli mbalimbali ambazo sio nzuri.

“Sababu kuwa ni kwamba hawajui misingi ya Muungano iliyowekwa na waasisi wetu, hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais inalojukumu kubwa la kutoa elimu kwao,” amesema Dk Shein.

Ikumbukwe Aprili 22, 1964 ndio siku ambayo hati ya Muungano ilisainiwa katika Ikulu ya Zanzibar na aliyekuwa Rais wa Tanganyika Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amman Karume.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button