Serikali yaibana Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi

SERIKALI imeiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma itimize wajibu wake ili kumaliza tuhuma dhidi ya viongozi wa serikali. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Ridhiwani Kikwete ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba na watendaji wa sekretarieti hiyo Dodoma.

Amesema sekretarieti ina jukumu la kikatiba la kumuita kiongozi anayetajwa hadharani au mafichoni kueleza ukweli wa taarifa zinazotolewa kwa kuwa nchi haiwezi kuwa na kila mtu anayeweza kusema wakati wao wanatakiwa kushughulikia hayo.

Amesema sekretarieti hiyo ina wajibu wa kuwaita viongozi, kutoa taarifa ambazo wananchi wanatakiwa kujua kwa sababu ni moja ya kusafisha serikali kwani hawawezi kuendelea kuwa na serikali ambayo viongozi wanalalamikiwa na wapotofu wa maadili wakawa wamekaa kimya.

“Nikakutumia wewe Waziri Mkuu kama mfano wa viongozi ambao uadilifu wake hauna kinga yoyote, niliwaambia hawa haiwezekani leo Waziri Mkuu anasimama kueleza katika maana ya kujisafisha juu ya umiliki wa mabasi ambayo tunajua kitaarifa na kitakwimu kuwa mabasi hayo si yake,” alisema Ridhiwani.

Amesema si utaratibu wa kiongozi kujisimamia mwenyewe kujitolea taarifa, kwani haitotokea hata siku moja mtu anayejisimamia kujitetea akaeleweka, wakati wao kama Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wamenyamaza kwa sababu hawaoni kama hiyo ni kazi yao.

Ridhiwani amesema hata yeye anashutumiwa kuhusu mambo ambayo anajua si yake na waliopewa kazi hiyo wanajua, lakini wameamua kunyamaza. Pia, amesema sekretarieti imepewa mwanya wa kuita chombo na kuomba taarifa popote wanapoona. SOMA: Mwigulu: Fanyeni mapitio tamko la mali, madeni

Na ili taarifa hizo zipatikane, wanatakiwa kuwaita wenzao wa vyombo vingine kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), idara za uchunguzi hata Jeshi la Polisi. “Rais ametoa maelekezo kuona nchi yake inakuwa yenye viongozi waliojaa maadili pia kuwaweka pembeni wanaokosa maadili tume hii ikitoa taarifa ikisema Ridhiwani ananuka rushwa wakimpelekea Mheshimiwa Rais ataupokea kwani ushauri wa tume hii ni sheria,” alieleza Ridhiwani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button