Ushirikiano unahitajika kuokoa maisha ya watoto njiti

MTOTO njiti ni mtoto anayezaliwa kabla ya muda wa kawaida wa mjamzito kujifungua wa wiki 37 za ujauzito. Inakadiriwa watoto njiti milioni 13.4 walizaliwa mwaka 2020, ikiwa ni takribani mtoto mmoja kati ya 10.

Ripoti iliyochapishwa mwaka jana na jarida la masuala ya afya la Lancet inaeleza kuwa, asilimia 65 ya watoto njiti waliozaliwa mwaka 2020 walitokea Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia Kusini. Ripoti inabainisha kuwa, nchi zilizoathiriwa zaidi ni Bangladesh asilimia 16.2, Malawi 14.5 na Pakistan 14.3.

Utafiti huo umeonesha suala la watoto njiti si la nchi tajiri au masikini, bali wajawazito wote wanaweza kuathirika katika kila kona ya dunia. Inafafanua kuwa takwimu zinazoonesha uwepo kwa idadi kubwa ya watoto njiti katika nchi tajiri, zikiwemo Ugiriki asilimia 11.6 na Marekani asilimia 10.

Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025-2050 inaelekeza kuendelea na jitihada za kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kuhakikisha uwepo wa vifaatiba na wataalamu wenye ujuzi zaidi katika afya ya mama na mtoto.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa kumekuwa na changamoto ya kuwapatia matunzo watoto njiti, hasa kwa wazazi wanaotoka maeneo ya vijijini. Kwamba, baadhi yao wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na mazingira duni na hivyo, kushindwa kuwatunza.

Mkazi wa Kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga, Lucy Maganga analieleza HabariLEO kuwa, baada ya kujifungua alikaa chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya kwa wiki mbili na baadaye akaruhusiwa kwenda kumlea mwenyewe nyumbani.

Maganga aliyejifungua njiti mwenye uzito wa kilo moja, anasema katika historia yake amekuwa na watoto wanne na wote amejifungua wakiwa njiti na wanaishi, isipokuwa mmoja ndiye alifariki. Anasema watoto waliobaki wana afya na wameshaanza shule. Anasema changamoto pekee ambayo mzazi anakutana nayo ni katika ukuaji wa taratibu wa mtoto katika kuongezeka uzito.

Anasema kwa uzoefu wake, amegundua hata hatua za mtoto kukua huchelewa ukilinganisha na waliozaliwa katika muda kamili. “Japokuwa sasa anakaa vizuri na chakula anakula vizuri, ipo changamoto ya kumlea mtoto iliyokuwa ikimlazimu kumbeba kwa njia ya kumweka tumboni (kangaroo) kama wanavyoelekeza wataalamu, muda wa mchana na usiku kumweka juu ya kifua kuhakikisha baridi kali haimpati,” anasema Maganga.

Naye Mkazi wa Ibadakuli katika Manispaa ya Shinyanga, Sesilia Madigo anasema kumtunza mtoto njiti ni changamoto kubwa. Anasema kabla ya kuingia utaalamu wa vifaa hospitalini, walikuwa wanatumia njia za kienyeji za kumwogesha mafuta ya nazi mtoto, badala ya maji ili kumuongezea joto.

Katika kuhakikisha usalama wa watoto njiti, serikali imeendelea kufanya jitihada kuweka mazingira wezeshi katika malezi yao. Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Santiel Kirumba anasema serikali imeweka huduma ya mtoto njiti katika huduma za bima.

Anasema kilichobaki ni kutazama namna ya kufanya marekebisho katika suala la likizo ya uzazi kwa mama aliyeajiriwa aliyejifungua mtoto njiti ili aongezewe muda. Santiel anasema, “Mjamzito akijifungua ana miezi sita, itamtaka akae siku 90 ili mtoto aweze kutimia lakini kunahitaji huyu mama aongezewe likizo ya uzazi,” anasema Santiel.

Santiel anasema mama anapokuwa katika kulea mtoto njiti, ni gharama na inaweza kumfanya mwanamke arudi nyuma kiuchumi, kwa sababu anatumia muda mwingi kumwangalia mtoto zaidi kuliko kufanya shughuli za kumwingizia kipato. SOMA: Mbio za Meru Pazuri kusaidia watoto njiti

Anapongeza serikali kwa juhudi inazofanya kuboresha sekta ya afya kwa kupeleka Sh milioni 157 kununua vifaatiba na kujenga jengo la mtoto njiti katika Mkoa wa Shinyanga. Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk John Luzila anasema wastani wa watoto 30 huzaliwa katika hospitali hiyo wakiwa chini ya wiki 37, hali inayothibitisha ukubwa wa changamoto hiyo katika jamii na serikali kuweka jitihada za kuwafanya waendelee kukua.

Katika maadhimisho ya Siku ya Watoto Njiti Duniani, Dk Luzila anasema kuanzia mwezi Januari hadi Oktoba 2025, watoto njiti 315 wamepatiwa huduma na hali zao zinaendelea vizuri. Anasisitiza wazazi kuendelea kuwa makini katika malezi ya watoto hao. Kwa mujibu wa Dk Luzila, maboresho ya huduma za watoto wachanga yameiwezesha hospitali hiyo kuokoa maisha ya watoto waliozaliwa na uzito mdogo kati ya gramu 600, 800 hadi 900, hali ambayo katika miaka ya nyuma ilikuwa nadra kutokea.

“Hatua hii ni ushindi mkubwa unaotokana na juhudi za watumishi, wazazi na uwekezaji wa serikali katika huduma za watoto wachanga na changamoto nyingine zinaendelea kushughulikiwa, ikiwemo upatikanaji wa vifaa muhimu vya watoto njiti,” anasema. Dk Luzila anasema kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO), kati ya wanawake 10 wanaojifungua, mmoja hujifungua mtoto njiti anayehitaji huduma maalumu na ufuatiliaji wa karibu.

Dk Martha Munuo wa Idara ya Watoto na Afya ya Uzazi anataja baadhi ya changamoto zilizopo kuwa ni pamoja na upungufu wa mashine za upumuaji (CPAP), Wazazi wakiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga wakipatiwa elimu kuhusu malezi kwa watoto njiti,dawa za kukomaza mapafu, udogo wa wodi na upungufu wa watoa huduma katika Wodi Maalumu ya Watoto Njiti (NICU).

Dk Munuo anasema mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia hospitali hiyo ni pamoja na uokoaji wa watoto waliozaliwa na uzito wa gramu 600 hadi 900 kupitia huduma za NICU. Nyingine ni ushirikiano wa wazazi waliokubali kufanya kangaroo pamoja na ushirikiano wa wadau wa afya.

Serikali ya Tanzania imeelekeza hospitali zote nchini kuwa na huduma za uangalizi maalumu kwa watoto njiti, kwa kuwa asilimia 70 ya wajawazito wanajifungua katika zahanati na vituo vya afya. Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inaelekeza kuendelea kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuhakikisha wajawazito wanajifungulia katika vituo vya afya kwa kusaidiwa na wataalamu wenye ujuzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button