Aahidi kiwanja, gari kwa watumishi wa serikali akiwa rais

DAR ES SALAAM: MGOMBEA Uraisi kupitia Chama cha Wananchi CUF, Gombo Samandito Gombo ameahidi kuwa endapo Watanzania watampa ridhaa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atahakikisha kuwa watumishi wa serikali wanatapatiwa barua ya ajira itakayoambatana na hati ya kiwanja pamoja na usafiri (gari).

Gombo amesema hayo wakati akifanya mahojiano maalumu na Daily News Digital, ambapo mgombea huyo ameeleza vipaumbele vyake kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Amesema lengo la kuja na mpango huo ni baada ya kuona watumishi wa serikali wanaishi maisha ya kawaida jambo linalochochea kuwepo kwa mianya ya rushwa kwa baadhi ya watumishi hao.

“Ukitaka kupunguza rushwa nchi hii, tumeshaona rushwa inatokea kwa utaratibu gani, kama mtu anahitaji nyumba au gari na ni mfanyakazi wa serikali inafika mahali ili aweze kuvipata hivyo vitu lazima ajihusishe na rushwa au ameuguliwa ni lazima afanye rushwa ili akamtibie mgonjwa wake, lakini kama serikali itatoa vitu hivyo bure tutakuwa tumezuia rushwa” amesema mgombea huyo.

Gombo ameongeza kuwa “Tukishakupa ile barua ya ajira, tutakupa na hati ya kiwanja, suala la nyumba tutalitatua palepale, kuna mabenki mengi yanatoa mikopo, tukishakupa hati yako na wewe ni mtumishi unaipeleka kule wanakujengea nyumba huku unailipia kidogo kidogo kupitia mshahara wako kwa muda wa miaka 15 na zaidi. Tunafanya hivi kwasababu wafanyakazi wengi hawana uwezo wa kujijengea nyumba, hivyo tunamuhakikishia kwamba anapoingia kazini anakuwa na nyumba.”

Aidha, amewaondoa shaka watumishi wa umma juu ya uwepo wa makato mengi kwenye mshahara wao, ambapo amesema kuwa katika serikali ya CUF itahakikisha inakomesha utitiri wa makato kwani baadhi ya mahitaji ya msingi itakuwa imewatimizia ikiwemo suala la afya.

“Tumeshaondoa suala la bima ya afya kwasababu tutatoa huduma za afya bure, hivyo ile pesa ambayo aliyokuwa anaitumia kwenye bima ya afya tayari tutakuwa tumeshamlipia kama serikali, na ndio maana tunasema katika serikali yetu mtu ataanza kula pensheni yake siku ya kwanza atakapoajiriwa na sio kusubiri kwa zaidi ya miaka 30 ili kujipatia mahitaji ya msingi kama nyumba” amesema mgombea huyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button