ACT- Wazalendo wang’aka Mpina ‘kunyolewa’

DAR ES SALAAM: CHAMA cha ACT Wazalendo kimepinga uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuzuia mgombea wake wa urais, Luhaga Mpina, kurejesha fomu za uteuzi, kikidai hatua hiyo ni kinyume cha Katiba na inaleta mashaka kuhusu uhuru wa tume.
Barua ya Agosti 27, 2025, iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Ado Shaibu, chama hicho kimeeleza kushangazwa na barua ya INEC ya Agosti 27, 2025 iliyotokana na nakala ya barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyotangaza kutengua uteuzi wa Mpina.
“Maamuzi haya sio tu kwamba ni ya aibu bali yanaibua maswali mengi juu ya uadilifu, umakini, uweledi na uhuru wa tume ambayo imepewa dhamana ya kikatiba kuwa huru,” imedai sehemu ya barua hiyo.
ACT Wazalendo imedai kuwa tayari mgombea wake alishapewa fomu na Tume Agosti 15, 2025, akazijaza, kupata wadhamini na kuhakikiwa kama taratibu zinavyotaka.
Urejeshaji wa fomu na uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais unafanyika leo katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zilizopo eneo la Njedengwa, Dodoma.
Mchakato huo unafanyika kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 50 na 62 vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, vikisomwa pamoja na kanuni ya 23 na 26 za Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025.