ACT-Wazalendo yapinga INEC kumuondoa Mpina

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema hakikubaliani na uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumuondoa mgombea wake wa urais, Luhaga Mpina katika kinyang’anyiro hicho.

ACT-Wazalendo imeeleza hayo kupitia taarifa yake kwa umma na kueleza Septemba 15, mwaka huu chama hicho kilipokea taarifa ya INEC ikiwasilisha uamuzi wake kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wagombea wa urais wa vyama vya AAFP na NRA dhidi ya mgombea wao.

Pia, chama hicho kimesema kimepokea uamuzi wa INEC kuhusu pingamizi la Mpina dhidi ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan.

SOMA: Aliyemshitaki Mpina agoma kung’oka ACT

Taarifa hiyo ya ACT-Wazalendo imeeleza katika barua ya INEC kuhusu pingamizi hilo, tume imelikataa bila kueleza sababu za kufanya hivyo kwa hoja zilizoelezwa na mgombea wao.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa chama hicho na mgombea hakubaliani na uamuzi wa tume kwa kuwa haujazingatia misingi ya sheria na kwamba mgombea wao hakutendewa haki.

“INEC imefanya maamuzi kwa kutumia uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa ambao chama na mgombea tumeukatia rufaa katika Mahakama Kuu kupitia shauri namba 23428 la mwaka 2025 Masijala Kuu Dodoma.

Kwa mujibu wa sheria, tume haikuwa na nafasi ya kuutumia uamuzi wa Msajili kufanya uamuzi wake dhidi ya mgombea wetu mpaka suala hii litakaposikilizwa na kuamriwa na mahakama,” imeeleza taarifa hiyo.

Chama hicho kimesema Kiongozi wa Chama hicho Taifa, Dorothy Semu ameitisha kikao cha dharura cha
Kamati ya Uongozi ya Taifa kujadili suala hilo.

Taarifa ilieleza pamoja na mambo mengine kikao hicho kitafikiria kuitishwa kwa Kikao cha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kwa madhumuni ya kuchukua uamuzi wa pamoja kisiasa na kuendeleza hatua za kisheria zilizopo.

INEC Septemba 15 ilitangaza kuondoa jina la Mpina katika orodha ya wagombea wa nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Taarifa ya INEC kupitia kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima ilisema hatua hiyo imefikiwa kufuatia pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari dhidi ya uteuzi wa Mpina kugombea urais kupitia chama hicho.

Kwa mujibu wa Kailima, INEC ilipokea mapingamizi manne yaliyowasilishwa dhidi ya wagombea wa nafasi ya urais na kupitia kikao chake kilichofanyika jana ilifanya maamuzi ya kutupilia mbali mapingamizi matatu na kukubali hoja zilizotolewa na Johari hivyo kuamua kuondoa jina la Mpina kwenye orodha ya wagombea wa nafasi hiyo.

Aidha, Septemba 13, 2025 INEC ilimteua Mpina kugombea nafasi hiyo baada ya kurejesha fomu za kuomba uteuzi akiwa na mgombea mwenza, Fatma Fereji katika ofisi za INEC, Dar es Salaam.

Hii ni baada ya Septemba 11, 2025 Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Kuu Dodoma kuiamuru INEC kutoa fursa kwa Mpina kurudisha fomu na mchakato wa kupokea uendelee pale ulipoishia Agosti 27, mwaka huu.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. I am making a real GOOD MONEY ($100 to $120 / hr) online from my laptop. Last month I GOT cheek of nearly 19840$, this online work is simple and straightforward, don’t have to go OFFICE, Its home online job. You become independent after joining this JOB. I really thanks to my FRIEND who refer me

    This SITE….., http://Www.Cashprofit7.site

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button