ADA-Tadea kuwamilikisha wachimbaji wadogo ardhi

CHAMA cha ADA-Tadea kimesema serikali yake itarekebisha sekta ya madini kwa kuwawezesha wachimbaji wadogo na wamiliki wa maeneo yenye madini kupata haki ya kuwa na ardhi yao.

Ilani ya uchaguzi ya chama hicho imeeleza kuwa itawapatia mitambo ya uchimbaji madini na wataalamu kwa makubaliano maalumu ili kuwajengea uwezo wa kuwa wachimbaji wakubwa baadaye.

Imesema itashirikisha wataalamu wa madini ili kuhakikisha haki na wajibu wa jamii iliyo kwenye madini inalindwa na kufanyiwa kazi  kwa manufaa ya jamii yote.

SOMA: Tusikilize sera kwenye kampeni, wavuruga amani tuwakatae

“Ushirikiano mkubwa utafanyika sambamba na wataalamu wa madini kwa kutumia watu stahiki katika shughuli za uchimbaji na kupiga marufuku kwa ufuatiliaji ajira za watoto kwenye migodi,” imesema.

Ilani hiyo ilieleza kuwa serikali itahakikisha asilimia ya mapato yatokanayo na mchakato wa shughuli za madini na maliasili nyinginezo yatapelekwa kwenye sekta za elimu na afya kwa ajili ya kuziboresha kwa kuzifanyia mabadiliko ya kimkakati.

Kuhusu masuala ya leseni za uchimbaji wa madini, ADA-Tadea imebainisha kuwa serikali yake itaweka usajili wake wazi ambapo majina ya wawekezaji yatachapishwa na watawajibika kwa utendaji wao.

Kwa upande wa sekta ya ardhi, ADA-Tadea imeeleza kuwa itafanya mabadiliko katika upangaji wa matumizi ya ardhi kwa kupanga matumizi bora ya ardhi ili kupunguza kero za uvamizi wa maeneo na wananchi kuvunjiwa nyumba zao kwa kigezo cha kupanua barabara.

“Mipango Miji na Vijijini itapanga matumizi bora ya ardhi kwa weledi wa hali ya juu kiasi kwa kuangalia mbele kwa miaka 100 ijayo, uwezo wa kufanya hayo na wataalamu tunao, vifaa vipo ni suala la kuwajibika kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,’’ imesema.

Ilisema ni aibu kwa taifa kuwavunjia watu nyumba au kuharibu barabara iliyojengwa kwa fedha nyingi katika kipindi kifupi, hivyo ni muhimu kuwa na mipango ya maono ya muda mrefu.

Ilani hiyo ilisema itahakikisha kila Mtanzania anapewa kipande cha ardhi afikapo miaka 21 ambacho kitakuwa mali yake na hataruhusiwa kukiuza.

Itawekwa pia sheria ili iwe ni marufuku kwa miji na vijiji ifikapo mwaka 2030 kuwa na nyumba za nyasi, labda kwa sababu maalumu kama utamaduni, maonesho, kimila au matambiko lakini siyo malazi.

“Tutarekebisha sheria ya ndoa na talaka ili wanaume na wanawake wapate haki sawa kulingana na makubaliano.
Endapo kutakuwa na migogoro ya ardhi na mahakama imetupilia mbali mashauri, itaundwa timu maalumu ya kitaifa kushughulikia migogoro hiyo,’’ imesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button