Walii: Tazameni ujumbe wa filamu, si majina

DAR ES SALAAM : MUONGOZAJI wa filamu na msanii wa Tanzania, Adarus Walii, ameingiza sokoni filamu yake mpya iitwayo Mke wa Mama, ambayo sasa inapatikana katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo YouTube.
Walii, ambaye amewahi kutamba na filamu kama Muuza Genge, Aisha, Namtaka Mwanangu, Bondo DSM, Slay Queens na Mapenzi na Muziki, amesema filamu hiyo mpya inaleta mafunzo makubwa kwa jamii kupitia kisa kinachoendana na maisha ya kila siku.
“Filamu hii inamuhusu kijana aitwaye Walii ambaye anakumbana na changamoto zinazomsukuma mama yake kuamua kumuolea mke kwa niaba yake. Tukio hilo ndilo linaloleta taharuki na changamoto zaidi katika jamii,” alisema.
Ameeleza kuwa utofauti wa filamu hiyo ni ujumbe unaobeba hali halisi ya watu wanaochelewesha maamuzi na hatimaye kukumbana na madhara ya maamuzi yaliyofanywa na wengine kwa niaba yao.SOMA: Failmu ya FESTAC ‘77’ kuwakilisha Afrika Cannes 2025
Aidha, Walii alisema filamu hiyo imehusisha kwa kiwango kikubwa wasanii chipukizi ambao wameonyesha uwezo mkubwa, huku akiwataka mashabiki wa filamu kusapoti kazi hiyo kwa kuangalia maudhui na ujumbe wake badala ya kujikita kwenye majina ya wasanii.



