ADC yaja na mikopo kwa wanaume, afya, elimu bure

CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema serikali yake itavunja utaratibu wa mikopo kwa makundi fulani na itaanzisha mikopo kwa wanaume wenye majukumu ya familia.

Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho 2025-2030 imeeleza wanaume hao watapata mgao wa mikopo angalau asilimia 30 hadi 40 na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu watapewa sehemu zao.

ADC ilieleza takwimu zinaonesha wanaume wenye umri wa miaka 35-50 na kuendelea ni nguzo za kaya nyingi. Wanaume hao wanalipa ada za shule, gharama za afya na kulisha familia lakini mara nyingi husahaulika kwenye upatikanaji wa mikopo.

“Wanaume hawa mara nyingi tayari wana miradi inayoendelea, hivyo wakipata mtaji wanaongeza uzalishaji mara moja na kurejesha mkopo kwa ufanisi,” imeeleza ilani.

Imeongeza: “Sera ya sasa inayowapa kipaumbele wanawake na vijana pekee inaweza kuacha nyuma kaya ambazo mtoaji mkubwa wa kipato ni mwanaume asiye kwenye makundi hayo ya kipaumbele.”

ADC imeeleza mikopo itafanyiwa tathmini kulingana na kaya nzima bila kuzingatia jinsia pekee ya mwombaji na itatolewa kwa kuangalia kama mradi una tija, uendelevu na uwezo wa mwombaji kuurejesha.

“ADC itavunja mfumo wa sasa wa upendeleo wa mikopo kwa makundi fulani tu na kuanzisha sera ya ‘Mikopo kwa Wote’ ili kuhakikisha kila mwenye mradi unaoleta tija anapata mtaji bila kubaguliwa kwa jinsia au umri,” imeeleza Ilani.

Afya

Ilani imeeleza ADC inatambua afya bora ni msingi wa maisha na maendeleo ya taifa hivyo huduma za afya ni haki ya msingi kwa kila raia na si anasa.

Chama hicho kimeahidi kutoa matibabu ya bure kwa wananchi wote kuanzia zahanati za vijiji, hospitali za wilaya, mikoa hadi hospitali za rufaa za taifa.

 

“Kila Mtanzania atasajiliwa moja kwa moja kwenye mfumo wa bima ya afya ya umma, inayogharamiwa na serikali kupitia kodi za maendeleo. Serikali itahakikisha upatikanaji wa dawa, vifaatiba, vipimo na huduma za dharura bila upungufu,” imeeleza Ilani.

Imeongeza: “Chanjo, uchunguzi wa mapema wa magonjwa sugu (kama kisukari, shinikizo la damu, saratani) na kampeni za afya ya jamii zitatolewa bure ili kupunguza mzigo wa matibabu makubwa baadaye. Huduma zitatolewa kwa viwango sawa mijini na vijijini ili kupunguza pengo la huduma za afya kati ya maeneo tofauti ya nchi.”

Elimu

ADC imeahidi kutoa elimu bila ada au michango yoyote kuanzia shule ya awali, msingi, sekondari, vyuo vya ufundi hadi vyuo vikuu.

“Serikali itatoa bure vitabu, madaftari, sare na vifaa vya mafunzo ili kuhakikisha usawa wa fursa kwa wanafunzi wote. Wanafunzi wote watakaohitaji msaada wa kifedha kwa ngazi ya elimu ya juu watapata mikopo yenye masharti nafuu bila ubaguzi,” imeeleza Ilani hiyo.

Kilimo

ADC imeahidi kuwapatia wakulima mbegu bora, mbolea na pembejeo nyingine bila gharama za awali.

“Kodi italipwa baada ya mazao kuuzwa sokoni ili wakulima waongeze uzalishaji, kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa. Tutahakikisha tunayatafutia mazao ya kibiashara soko zuri ili wakulima waweze kunufaika na bidhaa zao” imeeleza Ilani.

Imeongeza: “ADC itaondoa kodi ya awali kwenye vifaa vya uvuvi kama nyavu, ngalawa, injini na barafu. Kodi italipwa baada ya samaki kuuzwa sokoni, ili kupunguza gharama za mwanzo na kuongeza upatikanaji wa mazao ya uvuvi”.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button