Afya ya udongo muhimu kabla ya kutumia mbolea


“ Rai yangu ni kwamba wakulima waendelee kupima afya ya udongo ili kuwa na uhakika wa kufanya kilimo endelevu , kilimo chenye tija ili tuweze kupata usalama wa chakula pamoja na kipato” amesema Kamhabwa.
Wakati huo huo ,Mtaalamu Mwandamizi wa Maabara kutoka Idara ya Sayansi ya Udongo na Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk Hellen Kanyagha amesema kuwa wakulima wanaolenga kilimo chenye tija ni vyema wahakikishe wanapima afya ya udongo pamoja na afya ya mbegu ili kuepuka hasara na kuongeza ufanisi wa uzalishaji.
Dk Kanyagha amesema hayo katika Banda la Chuo Kikuu hicho alipokuwa akitoa elimu kwa wakulima juu ya huduma ya upamaji wa udongo, afya ya mimea na mbegu.
“Kwanini ni muhimu mkulima kupima udongo, kwa sababu inamsaidia kufahamu kiasi cha virutubisho kilichopo katika udongo”amesema
“ Pia inampa uwezo wa kujua aina ya mbolea anayotakiwa kutumia na aina gani ya virutubisho vinatakiwa kuongezwa kwenye udongo wake ili aweze kulima kwa tija na kupata mazao bora na yenye afya bora,” amesisitiza Dk Kanyagha.
Kwa upande wa mbegu, alisema kuwa mkulima anapoangalia afya ya mbegu anazotumia atakuwa na uhakika wa mbegu anayopanda inaota kwa kiasi gani shambani na kumpatia mavuno ya kutosha .



