Ajali yaua wawili Morogoro, dereva atoroka

MOROGORO: JESHI la Polisi linamtafuta dereva wa basi la Kampuni ya Kasulu Express aliyekimbia baada ya kusababisha ajali iliyoua watu wawili na kujeruhi kadhaa iliyotokea katika kijiji cha Kwambe kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Ajali hiyo imetokea Februari 26, 2025 majira ya saa 5 asubuhi katika kijiji hicho baada ya basi hilo kuacha njia na kupinduka wakati akijaribu kulikwepa gari lingine.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama, imeeleza kuwa watu hao waliokufa bado hawajatambuliwa ambao ni mtoto na mwanamke mmoja.
“Maiti zimepelekwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya utambuzi huku idadi ya majeruhi inaendelea kufuatiliwa,” amesema Mkama.
Aidha, kamanda huyo amesema dereva wa gari hilo lingine Munyabungingo Viateur ,38, ambaye ni mkazi wa Kigari nchini Rwanda anashikiliwa kwa ajili ya mahijiano zaidi.



